Taasisi ya kutetea haki za binadamu ya Palestina imetangaza kuwa, tangu mwaka 1967 hadi sasa Wapalestina 73 wameaga dunia kutokana na upuuzaji unaofanywa na Israel wa kutowapatia matibabu stahiki mateka wa Kipalestina katika jela za utawala huopandikizi unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Klabu ya wafungwa ya Palestina jana Jumapili imeripoti kuwa, raia hao 73 wa Palestina ni sehemu ya mashahidi 231 wa harakati ya wafungwa wa Kipalestina waliopoteza maisha tokea mwaka 1967; na Israel inaendelea kuzuia miili ya wafungwa 9 ambao waliaga dunia wakiwa kifungoni.
Klabu ya wafungwa ya Palestina imeongeza kuwa, suala la wafungwa wagonjwa ni kadhia ambayo limekuwa mada kubwa katika miaka ya karibuni kwa sababu jinai zinazotokana na uzembe wa kimatibabu au mauaji ya taratibu na vile vile sera za utesaji zinadhihirisha sera kuu zinazotekelezwa na utawala ghasibu wa Kizayuni na kusababisha vifo vya wafungwa.
Aidha hivi sasa karibu wafungwa 600 wa Kipalestina wagonjwa wamefungwa katika jela mbalimbali za Israel huku wakiishi katika hali ngumu. Takriban wagonjwa 200 kati yao wanaugua magonjwa mbalimbali sugu na 23 wanaugua uvimbe na saratani.
Klabu ya wafungwa wa Palestina imezituhumu seli na magereza yanayowashikilia wafungwa na mateka wa Kipalestina kwa kukataa kwa makusudi kuwapeleka hospitali wafungwa wagonjwa na kutowafanyia vipimo ili kubaini maradhi yao.