Mazoezi ya Uwezo 1401 ya jeshi la Iran yanafanyika kwa muda wa siku mbili kwa lengo la kutathmini na kuboresha kiwango cha nguvu na utayari wa kupambana wa Jkikosi cha Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kukabiliana na vitisho tarajiwa.
Mazoezi hayo yalianza jana Jumatano kwa kushirikisha askari wa miguu, drone, kituo cha uhandisi na vitengo vya vita vya elektroniki kwa msaada wa ndege wa Jeshi la Anga na yataendelea kwa siku mbili katika eneo la Nasrabad, huko Isfahan.
Msemaji wa maneva hayo ya Jeshi la Nchi Kavu Brigedia Jenerali Cheshak, amesema: Katika mazoezi haya ya siku mbili, kunafanyiwa tathimini ya operesheni za kuhamisha haraka askari kutoka baadhi ya maeneo hadi maeneo mengine, kuboresha operesheni ya kusafirisha haraka brigedi za vikosi maalumu na majibu ya haraka, utekelezaji wa mbinu mbalimbali, kiwango cha uratibu katika utekelezaji wa operesheni za pamoja za vikosi vya jeshi na kadhalika.
Kufanyika kwa mazoezi haya ya Jeshi la Nchi Kavu ni onyo kubwa kwa maadui wa Iran ya Kiislamu na wakati huo huo ishara nyingine ya utayarifu wa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya kulinda ardhi ya Iran na usalama wa taifa kwa kwa kutilia maanani vitisho vya hivi karibuni vya maadui hususan utawala wa Kizayuni wa Israel unaoungwa mkono na Marekani.
Meja Jenerali Gholam Ali Rashid, kamanda wa Kituo Kikuu cha jeshi cha Khatamul Anbiya ameashiria matamshi rasmi yaliyotolewa na maafisa watendajinai wa utawala wa Kizayuni wa Israel na vitisho vyao dhidi ya vituo vya nyuklia vya Jamhuri ya Kiislamu, maslahi na usalama wa taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutangaza kuwa: Utawala wa Kizayuni ndio unaopewa kipaumbele cha kwanza kama tishio kwa usalama wa taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Meja Jenerali Rashid amesema: “Kwa mtazamo wa kituo hicho cha Khatamul Anbiya, vitisho vyovyote vya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya maslahi na usalama wa taifa wa Iran vitatathminiwa kwa kuzingatia taarifa, uratibu na uungaji mkono wa Marekani, na jibu la vikosi vya jeshi la Iran litakuwa la uhakika na kwa kiwango sawa. Vilevile mamluki na nchi zote zinazoshirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel kutishia usalama wa taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, zitalipa gharama ya hatua hiyo.”
Kwa miaka mingi, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitishia kushambulia taasisi za kuzalisha nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani nchini Iran kutokana na maendeleo yaliyopatikana hapa nchini katika sekta hiyo, huku ukijua vyema kwamba ni dhaifu sana na hauwezi kustahamili majibu ya kulipiza kisasi ya Iran. Mtaalamu wa masuala ya kisiasa, Zohir Andraus anasema: “Wataalamu na wachambuzi wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanasisitiza kwamba, utawala huo hauna uwezo wa kuishambulia Iran. Hatua kama hii inahitajia miaka kadhaa, na iwapo Israeli itaanzisha shambulio kama hilo, itakabiliwa na uharibifu na maangamizi yasiyo na kifani.”
Wakati huo huo, Iran ya Kiislamu, na kwa kutilia maanani amri ya Qur’ani ya kujizatiti kwa zana za kujihami na uwezo wa kukabiliana na adui kwa ajili ya kumtia woga na wahka, imefanikiwa kuunda zana za kisasa kwa kutumia ujuzi na wataalamu wa ndani. Vilevile vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vikiwemo vikosi vya Jeshi la Nchi Kavu, vimeongeza maandalizi yao ya ulinzi kwa kufanya maneva ya kijeshi na vimedhihirisha uwezo wa kijeshi wa Iran dhidi ya maadui.
Meja Jenerali Rashid anaashiria maoezi ya Jeshi la Nchi Kavu la Iran na kusema: Makamanda wa vikosi vya ardhini vya jeshi la Iran wanafuatilia kikamilifu nyendo za adui na wako kwenye utayarifu wa hali ya juu zaidi wa kutumia nguvu na kukabiliana na uchokozi na vitisho vyake. Meja Jenerali Rashid ameongeza kuwa: Maozezi ya “Uwezo wa Vikosi vya Jeshi la Nchi Kavu 1401” yamepangwa na kutekelezwa kwa mujibu wa vita vijavyo na vitisho tarajiwa.