Mazungumzo ya Mawaziri wa Ulinzi wa Imarati na Syria mjini Damascus yaikasirisha Washington

Washington imetoa radiamali kufuatia ziara ya karibuni ya Waziri wa Ulinzi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) mjini Damascus na kutishia kuwa, hatua yoyote ya Imarati kuhuisha uhusiano na serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria itazigharimu pande mbili hizo.

Abdullah bin Zayed Al Nahyan Waziri wa Ulinzi wa Imarati hivi karibuni alifanya ziara ambayo ni ya pili kuwahi kufanywa na waziri huyo wa Umoja wa Falme za Kiarabu huko Damascus ikiwa ni katika juhudi za pande mbili za kuboresha uhusiano kati yazo.

Katika ziara hiyo, Mawaziri wa Ulinzi wa Syria na Imarati walijadili suala la kuhuisha uhusiano na kukuza ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi mbili huku Rais Assad wa Syria akisema kuwa, uhusiano huo utasaidia uthabiti katika eneo.

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi wa Imarati Sheikh Abdullah ambaye aliongozana na kundi la maafisa wa masuala ya uchumi na usalama katika ziara yake hiyo huko Damascus ameeleza kuwa anaunga mkono kupatiwa ufumbuzi mgogoro wa Syria kwa njia za kidiplomasia.

Uhusiano kati ya Syria na UAE uliharibika baada ya Syria kufukuzwa katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yenye wanachama 22 (Arab League) mwaka 2011. Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ulifungua tena ubalozi wake huko Syria mwaka 2018. Bahrain, Algeria na Jordan pia zimeanzisha tena uhusiano na Syria huku mataifa mengine ya Kiarabu yakitoa wito wa kurejeshwa Syria katika jumuiya ya Arab League.

Hatua zote hizi hazijaifurahisha Washington kwa sababu viongozi mbalimbali wa Marekani wamekosoa ziara ya karibuni ya Sheikh Abdullah mjini Damascus huku Seneta mmoja wa Marekani  akitoa vitisho vya kuwekewa vikwazo Imarati kupitia ujumbe aliotuma katika ukurasa wake wa twitter.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *