Mazungumzo ya Maziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Afrika Kusini

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian amefanya mazungumzo ya simu na kubadilishana mawazo na Bi. Naledi Pandor, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, kuhusiana na masuala ya uhusiano pande mbili, kikanda na kimataifa.

Akigusia umuhimu wa Bara la Afrika katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza azma kubwa ya serikali ya Iran ya kuendeleza uhusiano na bara hili hususan na Afrika Kusini.

Huku akiashiria maandalizi ya kufanyika kwa kikao cha Kamisheni ya 15 ya Pamoja ya Uchumi ya nchi hizo mbili, Amir-Abdollahian ameeleza matumaini yake kuwa fursa na uwezo mwingi wa nchi hizo mbili utatumiwa zaidi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amepongeza misimamo ya Afrika Kusini kuhusu suala la Palestina na sera ya nchi hiyo ya uungaji mkono kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.

Aidha Amir-Abdollahian ameashiria kadhia ya  vita vya Ukraine na kusema: Tunaendelea na jitihada zetu za usitishaji vita nchini Ukraine na msimamo wetu ni kupinga vita na kumaliza mgogoro wa Ukraine kwa njia za kisiasa.

Kwa upande wake Bi. Naledi Pandor, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afrika Kusini pia ameashiria nafasi muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na amepongeza juhudi za kufanyika duru mpya ya Kamisheni ya Pamoja ya Uchumi ya nchi hizo mbili.

Huku akiashiria nafasi muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika upatanishi wa mgogoro wa Ukraine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesisitiza kuwa: Usitishaji vita ni muhimu kwa pande zote na jumuiya ya kimataifa, kwa sababu matokeo ya vita hivyo yamesababisha mgogoro wa chakula na nishati katika baadhi ya nchi. Aidha ameelezea matumaini yake kwamba mgogoro wa Russia na Ukraine utapatiwa ufumbuzi kupitia mazungumzo.

Pia ametumai kuwa mazungumzo ya nyuklia ya Iran yatakamilika haraka iwezekanavyo.

Bi. Pandor, pia ametilia mkazo mwaliko wa Rais wa Afrika Kusini  kwa Rais wa Iran kutembelea Pretoria na ameelezea matumaini yake kuwa ziara ijayo ya Rais wa Kiislamu wa Iran nchini Afrika Kusini itakuwa msingi wa  kuimarika zaidi mahusiano ya nchi mbili.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *