Mbunge wa Kizayuni afichua: 2023 Saudia na Israel zitasaini mkataba wa kuanzisha uhusiano rasmi

Mbunge wa chama cha Likud katika Bunge la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel amesema, kwa kuzingatia mazungumzo yaliyofanyika, inatarajiwa kuwa makubaliano ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya utawala huo na Saudi Arabia yatasainiwa mwaka ujao wa 2023.

Danny Danon, mbunge wa chama cha Likud kinachoongozwa na Benjamin Netanyahu, aliyekabidhiwa jukumu la kuunda baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni, amefichua kuwa makubaliano ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Israel na Saudia yanatarajiwa kusainiwa rasmi mwakani.

Tovuti ya gazeti la Kizayuni la The Times of Israel imemnukuu mwakilishi huyo wa zamani wa utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa na kuandika kuwa, uvumi huo unatokana na “mazungumzo” yaliyofanyika hivi karibuni.

Danon hakuashiria hatua maalum zinazochukuliwa kwa sasa katika mwelekeo huo isipokuwa amedokeza tu kwa kusema: “waziri mkuu Benjamin Netanyahu ameliweka suala la kupanua ‘Mkataba wa Abraham’ katika moja ya vipaumbele vyake.”

Mbunge huyo wa bunge la utawala haramu wa Israel amebainisha pia kwamba, safari ya kwanza atakayofanya Netanyahu baada ya kushika rasmi wadhifa wa uwaziri mkuu itakuwa ni ya kutembelea Muungano wa Falme za Kiarabu, Imarati.

Kwa mujibu wa tovuti ya The Times of Israel,  utawala wa Kizayuni unaichukulia Saudi Arabia kama “zawadi nono” kwake huku ukitaka uhusiano wa kiusalama uliopo hivi sasa baina ya pande mbili uchukue mkondo rasmi wa kidiplomasia.

Mnamo mwezi Julai mwaka huu, Saudi Arabia ilitangaza kuwa itafungua anga yake kwa ndege zote za kibiashara. Hata hivyo uamuzi huo wa Riyadh ulionekana kuulenga moja kwa moja utawala wa Kizayuni wa Israel kwa sababu ndio pekee uliokuwa hauna kibali cha kupitisha ndege zake juu ya anga ya Saudia.

Hayo yamejiri katika hali ambayo, kwa mtazamo wa wachambuzi na wachunguzi wengi wa masuala ya kisiasa, mchakato wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Tel Aviv na Riyadh ulishaaanza tokea muda mrefu nyuma.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *