Mchambuzi: Wafanyakazi wa Kiafrika wanakandamizwa sana Saudia

Haki za wafanyakazi wahamiaji wa Kiafrika zinapuuzwa kwa kiwango kikubwa Saudia Arabia na utawala huo wa kifalme wenye kiburi.

Zaakir Ahmed Mayet alisema hayo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Press TV siku ya Jumapili baada ya kanda za video kufichua mauaji ya wahajiri wa Kiafrika kutoka Ethiopia yanayofanywa na wanajeshi wa utawala wa Saudia iliyotolewa mapema mwezi huu.

Picha hizo zilionyesha kaburi la umati lililokuwa na makumi ya wafanyikazi wa Kiafrika waliouawa na walinzi wa mpaka wa Saudi. Wahajiri wa Ethiopia waliithibitishia kanali ya habari ya al-Masirah ya Yemen kwamba walinzi wa mpaka wa Saudi wanaua takriban wahajiri watano kwenye mpaka kila siku na kujeruhi wengine wengi.

Zakir Ahmed amesema, takriban asilimia 80 ya wafanyakazi katika sekta ya kibinafsi nchini Saudi Arabia ni raia wa kigeni na wahamiaji wa kigeni na wanakabiliwa na mateso makubwa.

Akifafanua kuhusu nukta hiyo amesema, “Watu hawa wanafanya kazi kwa muda mrefu zaidi ya saa 12 kwa siku, mishahara yao inacheleweshwa na wanaendelea kufanyiwa ukatili wa kijinsia pamoja na kubakwa na waajiri wao ndani ya Saudi Arabia.”

Mchambuzi huyo amesema “Utawala wa Saudi unageukia “nchi ya Kishetani”, kwani haki za wafanyikazi ziko chini kabisa katika ajenda ya ufalme huo.”

Licha ya kuwa miongoni mwa nchi tajiri zaidi, Saudi Arabia ina rekodi mbaya ya haki za binadamu, ambapo imewaweka kizuizini maelfu ya wahajiri wa Kiafrika na kuwatendea unyama wa kutisha.

Ahmed alisema “utawala wenye kiburi wa Saudia” unaamini kuwa utajiri wa mafuta  unaipa haki ya kufanya ipendavyo, wakati ipendavyo na kwa yule imtakaye.

Aidha amesema Wasaudi wanaamini “kwa sababu tu [wahamiaji] wana ngozi nyeusi na wanatoka maeneo tofauti wana asili ya chini kuliko binadamu wa kawaida na hawana haki ya utu na heshima.”

Halikadhalika amesema madola ya Magharibi yana historia ndefu ya kupuuza jinai za kutisha na ukiukaji wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia kutokana na utegemezi mkubwa wa mafuta na uuzaji wa silaha wenye thamani ya mabilioni ya dola kwa ufalme huo utendao jinai.

 

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *