Nyota chipukizi wa mchezo wa tenisi ya mezani raia wa Lebanon amejiondoa katika mashindano ya Kombe la Dunia ya Tenisi ya Mezani Kwa vijana Chipukizi (WTT) baada ya kupangwa kumenyana na mchezaji kutoka Israel (Palestina inayokaliwa kwa mabavu).
Bissan Chiri binti wa miaka 11 kutoka Lebanon amekataa kucheza na mchezaji Mzayuni na kutangaza kuliunga mkono taifa la Palestina linalokabiliwa na dhulma za utawala haramu wa Israel.
Binti huyo ameungana na wachezaji wengine katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu ambao wanapopangwa katika mashindano mbalimbali kukabiliana na Israel hujitoa wakionyesha kutoitambua Israel na wakati huo huo kuonyesha himaya na uungaji mkono wao kwa Palestina.
Bissam alijitoa katika mashindano hayo ya tenisi ya mezani kwa vijana chipukizi yanayoendelea nchini Ureno baada ya kuelezwa kwamba, angemenyana na binti Mzayuni Elinor Davidov kutoka Israel katika mechi ya mtu mmoja mmoja.
Mapema mwezi huu Mohamed Ataya mcheza tenisi mwingine wa Lebanon alijiondoa katika mashindano ya kimataifa ya tenisi huko Cyprus baada ya kupangiwa kushindana na Mzayuni.
Wimbi la utawala ghasibu wa Israel kususiwa kimichezo limeongezeka katika miaka ya hivi karibuni ambapo wanamichezo hao wamekuwa wakipinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel.
Katika mashindano ya Olimpiki yaliyopita ya 2020 huko Tokyo Japan wanamichezo wa judo wa Sudan na Algeria walikataa kumenyana na wanamichezo wa Israel na kutangaza kuwaunga mkono Wapalestina.
Duru za Kizayuni zinaripoti kuwa, wanamichezo wa nchi za Kiarabu na Kiislamu wanaudhihaki utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwa kuendeleza mwenendo huo.