Mgogoro wa kiuchumi barani Ulaya; kushadidi ufakiri wa chakula na fueli Uingereza

Katika miezi ya hivi karibuni hali ya kiuchumi katika akthari ya mataifa ya bara Ulaya imezidi kuwa mbaya na kuzusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa wakazi wa bara hilo.

Sadiq Khan, Meya wa mji wa London ametoa indhari kuhusu kuweko msimu wa baridi usio na chakula wala joto majumbani.

Meya huyo wa jiji la London ametangaza kuwa, wananchi wa Uingereza kutokana na uhaba wa fueli wanaokabiliwa nao, msimu wa baridi mwaka huu hawatakuwa na budi isipokuwa kuchagua moja kati ya mawili; ima watumie pesa kununua fueli na hivyo kuzitia joto nyumba zao kwa ajili ya kukabiliana na baridi au watumie fedha walizonazo kwa ajili ya kununua chakula na hivyo kkuusalimika na njaa. Ingawa ameeleza kuwa, akthahri ya wananchi wa Uingereza hawana uwezo wa kutekeleza hata chaguo moja kati ya mawili hayo.

Takwimu zilizotolewa mwezi uliopita wa Julai na taasisi iitwayo Hatua ya Kitaifa ya Nishati Uingereza zinaonyesha kuwa, familia zaidi ya milioni nane nchini Uingereza zinakabiliwa na hatari ya kupatwa na changamoto ya ufakiri wa fueli. Inaelezwa kuwa, kutokana na kupanda kwa bei za nishati, ifikapo mwezi Oktoba, mwaka huu familia zipatazo milioni nane na laki mbili nchini Uingereza zinaweza zikapatwa na changamoto ya ufakiri wa fueli; na wastani wa malipo ya nishati nchini humo katika msimu wa baridi wa mwaka huu unaweza ukafika paundi 3,250.

Filihali, tatizo la uchumi linazidi kuchukua wigo mpana zaidi barani Ulaya. Takwimu zinaonyesha kuwa, mwenendo wa kukua uchumi umesimama au upo katika mkondo hasi huku kiwango cha ughali wa maisha na ukosefu wa kazi na ajira kikiwa kimeongezeka mno.

Karantini za muda mrefu katika kipindi cha kuenea maradhi ya Covid-19, kusimamishwa sekta kuu za uchumi na uzalishaji, maluumbano ya kisiasa, kuongezeka bajeti ya kijeshi, kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya maarufu kwa jina la Brexit na hivi sasa vita vya Russia na Ukraine na kuamua madola ya Ulaya ikiwemo Uingereza kufuata mkumbo wa siasa za Marekani dhidi ya Russia, ni mambo ambayo yanatajwa na weledi wa mambo kuwa, yameshadidisha matatizo ya kiuchumi katika mataifa ya bara hilo.

Takwimu zinaonyesha kuwa, kiwango cha mfumuko wa bei mwezi Juni mwaka huu nchini humo kilifikia 9.1%, ambacho ni cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 40 iliyopita. Viongozi wa Uingereza wana wasiwasi hivi sasa wakihofia kiwango hicho cha mfumuko wa bei kuweka rekodi mpya katika miezi ya usoni.

Andrew Bailey, Gavana wa Benki Kuu ya Uingereza ametangaza kuwa, uchumi wa nchi hiyo umo katika hali mbaya kabisa kuliko hata ilivyotabiriwa na wajuzi wa masuala ya kiuchumi, na mpaka kufikia mwishoni mwaka huu uchumi wa nchi utaingia katika hatua ya mdodoro, hali ambayo kwa uchache itadumu kwa miezi 15.

Licha ya kuwa baada ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya, wachambuzi wengi wa mambo walitahadharisha kuhusiana na kuwa mbaya hali ya uchumi wa nchi hiyo, lakini msambao wa virusi vya corona na vita vya Russia na Ukraine vimeifanya hali hiyo izidi kuwa mbaya.

Hali hiyo haiishii nchini Uingereza tu, kwani hali ya mambo katika mataifa mengine ya Ulaya ni mbaya pia. Viongozi wa Ujerumani wametoa indhari kuhusiana na kushadidi malalamikko ya kijamii. Akthari ya misaada ya kijamii yenye lengo la kupiga jeki na kupunguza ukali wa maisha imekatwa, huku msimu wa baridi ukiwa njiani.

Hali hiyo nayo imezusha wasiwasi miongoni mwa wananchi na hata viongozi wa Ujerumani. Pamoja na hayo yote, lakini viongozi wa Ulaya hawataki kubadilika kwani wangali wanafuata kibubusa siasa za Marekani hususan kuhusiana na vita vya Ukraine.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *