Miaka saba tangu kunyongwa Ayatullah Sheikh Nimr Baqi al-Nimr mwanazuoni mtajika wa Saudi Arabia

Ayatullah Sheikh Nimr Baqi al-Nimr alikuwa mwanazuoni mahiri na mtajika wa eneo la Qatif mashariki mwa Saudi Arabia ambaye kwa kuunga mkono maandamano ya amani ya eneo hilo alikuwa akitaka kukomeshwa ubaguzi dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, na wakati huo huo kufanyike mageuzi katika mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Utawala wa Saudia ambao ulikasirishwa mno na hatua ya Ayatullah Nimr ya kuunga mkono maandamano ya wananchi, ulimtia mbaroni Julai 2012 kwa kutumia mabavu na nguvu kupita kiasi.

Baada ya kupita mwaka mmoja, serikali ya Saudia ilimhukumu adhabu ya kifo mwanazuoni huyo bila ya kuitaarifu familia yake na tarehe Pili Januari mwaka 2016 ikamnyonga pamoja na watu wengine 46 kwa tuhuma za kuhatarisha usalama wa taifa. Si hayo tu bali utawala wa Saudia ulikataa kukabidhi mwili wa shahidi huyo kwa familia yake baada ya kumnyonga.

Kunyonga mwanazuoni huyo wa Kiislamu ilikuwa moja ya ishara za wazi kabisa kwamba, mfumo wa kisiasa wa Saudi Arabia unatumia nguvu na ukandamizaji kupita kiasi. Ayatullah al-Nimr si tu kwamba, hakuchukua hatua yoyote ya kubeba silaha kwa ajili ya kukabiliana na utawala wa kifamilia wa Saudia, bali alichokifanya ni kuunga mkono tu maandamano ya wananchi.

Kama alivyosema, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ni kuwa: “Tatizo la Sheik al-Nimr ni kuwa alikuwa akipaza sauti ya kupigania haki. Alikuwa mtu shujaa. Alikuwa akisema maneno yake kwa ukakamavu na bila ya woga wowote. Alikuwa mpigania mageuzi na haki za wananchi wa Bara Arabu na alichokuwa akikitaka ni uhuru wa kawaida ambao anaouhitajia mtu yeyote katika pembe yoyote ile ya dunia.”

Kunyongwa Ayatullah Sheikh Nimr Baqi al-Nimr kulikuwa kwa kidhulma kiasi kwamba, hata waitifaki na washirika wa Saudia waliitaja hatua hiyo kuwa si ya kiakili. Hillary Clinton, ambaye wakati huo alikuwa mgombea wa kiti cha Urais kwa tiketi ya Wademokrati nchini Marekani alisema: “Sidhani kama hatua ya watawala wa Saudia ilikuwa ya busara.”

Chuo cha Foundation for Defense of Democracies kilitoa ripoti iliyoandikwa na David Andrew Weinberg ikieleza kwamba: “Kunyongwa Sheikh Nimr ni ukandamizaji unaotokana na mfumo wa kidikteta.”

Aidha jarida la Kijerumani la Bild liliandika kichwa cha habari katika chapisho la kesho yake baada ya kuuawa Sheikh Nimr: “Saudia haina kitu kingine kwa ajili ya walimwengu ghairi ya mafuta, tende na ugaidi.”

Miaka saba baada ya kuuawa shahidi Sheikh Nimr, jinai za utawala wa Aal Saud dhidi ya wananchi wa nchi hiyo hususan Waislamu wa madhehebu ya Shia zimechukua wigo mpana zaidi.

Idadi ya watu walionyongwa nchini humo mwaka jana imekuwa maradufu ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake yaani 2021.

Tarehe 12 Machi mwaka jana (2022) pekee, mamlaka za Saudia ziliwanyonga watu 81 kitendo ambacho kinahesabiwa kuwa unyongaji mkubwa wa umati katika historia ya nchi hiyo ya Kiarabu. Nusu ya wahanga wa siasa hizo za ukandamizaji walionyongwa siku hiyo walikuwa Waislamu wa madhehebu ya Shia, huku miongoni mwao wakiwa na umri mdogo. Wahanga hao hawakushtakiwa mahakamani rasmi na wala hawakuwa na mawakili wa kuwatetea.

Hapana shaka kuwa, kile ambacho kinawapa jeuri viongozi wa Saudia na kuendelea kufanya mauaji mchana kweupe ni kimya kinachoambatana na himaya na uungaji mkono wa madola ya Magharibi.

Kwa mfano, wakati watu 81 wananyongwa kwa umati nchini Saudia mwaka jana Machi 2022 madola ya Magharibi yalikuwa yameshughulishwa na vita vya Ukraine na harakati za kuibembeleza Riyadh iongeze kiwango cha uzalishaji mafuta.

Kwa kuzingatia himaya na uungaji mkono huo na bila kusahau kimya cha madola yanayodai kuwa vinara wa kutetea haki za binadamu ulimwenguni, si tu kwamba, walimwengu hawawezi kushuhudia kufikia kikomo ukandamizaji na utumiaji mabavu unaofanywa na mfumo wa kisiasa nchini Saudia dhidi ya raia wasio na hatia yoyote hususan Waislamu wa Kishia, bali wataraji kusikia matukio mengine ya kunyongwa kiholela na kwa umati watu huko nchini Saudia.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *