Mitambo ya ulinzi wa anga ya Syria yakabiliana na hujuma za Israel katika anga ya Damascus

Kikosi cha ulinzi wa anga cha Syria usiku wa kuamkia leo kimefanikiwa kunasa na kuteketeza makombora kadhaa ya adui mzayuni katika anga ya mji mkuu wa nchi hiyo Damascus.

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala ghasibu wa Israel umekuwa ukifanya mashambulio ya anga ya mara kwa mara katika mji mkuu wa Syria Damascus na maeneo mengine tofauti ya nchi hiyo, ambayo mara nyingi yamekuwa yakizimwa kwa wakati na mitambo ya ulinzi wa anga ya Syria.
Duru moja ya jeshi imeliambia shirika la habari la Syria SANA ya kwamba, mnamo saa nane za usiku wa kuamkia leo Jumatatu, utawala wa Kizayuni ulifanya mashambulizi ya anga kwa kurusha makombora kadhaa kutokea kaskazini mashariki mwa Ziwa Tiberias, yaliyolenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Damascus na maeneo ya kandokando yake.
Duru hiyo imeongeza kuwa, katika uchokozi huo, wanajeshi wawili wameuawa na wengine wawili wamejeruhiwa, na utoaji huduma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Damascus pia umevurugwa.
Takriban wiki mbili zilizopita utawala wa Kizayuni ulishambulia pia maeneo ya karibu na Damascus kwa makombora kadhaa kutoka kaskazini-mashariki mwa Ziwa Tiberias, ambapo mitambo ya ulinzi wa anga ya jeshi la Syria iliyazima na kuteketeza baadhi ya makombora hayo.
Mashambulizi hayo ya anga ya Israel yanajiri wakati serikali ya Syria imeshatuma barua mara kadhaa Umoja wa Mataifa kulaani mashambulizi hayo na kutaka yakomeshwe.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *