Mizozo iliyoibuka baina ya Kenya na majirani zake kama Tanzania, Somalia, Uganda Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inatajwa kuwa na taathira hasi kwa biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Ripoti zinaonyesha kuwa, mauzo ya Kenya kwa nchi jirani za Uganda na Tanzania yamepungua tangu Oktoba mwaka jana huku kukiwa na uhusiano mbaya kati ya nchi hizo tatu za Afrika Mashariki.
Tovuti ya Kenyans.co.ke inaripoti kuwa, takwimu kutoka Ofisi ya Takwimu ya Kenya (KNBS) zinaonyesha kwamba, mauzo ya Kenya hadi Uganda yalipungua kutoka $61.5m hadi $49.2 kati ya Septemba na Oktoba 2023, huku mauzo ya nje ya Tanzania yakishuka kutoka $35.7m hadi $31.4m katika kipindi hicho, tovuti ilisema.
Serikali ya Rais William Ruto inalaumiwa kwa kile kinachoelezwa kuwa, kuzusha migogoro baina yake na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.
Licha ya kukanusha, Uganda imeishtaki Kenya kwa madai ya kuinyima leseni ya kuagiza mafuta kupitia bandari ya Mombasa.
Tanzania ilipiga marufuku kwa muda safari za shirika la ndege la Kenya Airways kati ya Nairobi na Dar es Salaam mapema mwezi huu ili kulipiza kisasi uamuzi wa Nairobi kunyima haki ya Air Tanzania kuendesha safari za mizigo kati ya nchi hizo mbili.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi amekanusha ripoti za kuzorota kwa uhusiano kati ya nchi hiyo na majirani zake, licha ya mizozo kadhaa ya hivi majuzi ambayo alisisitiza kuwa inatatuliwa kidiplomasia.
Kenya ina kesi inayosubiri ya usambazaji wa mafuta na Uganda na ni wiki iliyopita tu ilisuluhisha mzozo wa kusafiri kwa ndege na Tanzania.
Mapema mwezi huu, Sudan ilimrudisha nyumbani mjumbe wake baada ya Nairobi kumkaribisha mkuu wa Kikosi cha Msaada wa Haraka wa kijeshi Mohamed Dagalo, ambaye anahusika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na jeshi la Sudan.
Mwezi Disemba, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia ilimwita balozi wake mjini Nairobi baada ya muungano mpya wa waasi wa Kongo kuundwa katika mji mkuu wa Kenya.