Mke wa Rais wa Zimbabwe asisitiza kustawishwa uhusiano wa nchi yake na Iran

Mke wa Rais wa Zimbabwe amesisitiza juu ya udharura wa nchi yake kuimarisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mama Auxillia Mnangagwa ambaye yuko safarini hapa nchini amesema hayo katika mazungumzo yake mjini Tehran na Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Aidha amesema ana matarajio muda si mrefu kutafanyika kikao cha 9 cha kamisheni ya pamoja baina ya Iran na Zimbabwe na kwamba, nchi yake inathamini mno suala la kupanua ushirikiano wake na taifa la Iran.

Mama Auxillia Mnangagwa ametoa mwito wa kuweko ushirikiano jumuishi wa kiuchumi baina ya Zimbabwe na Iran katika nyuga mbalimbali kwa shabaha ya kuimarisha ushirikiano baina ya pande mbili.

Kwa upande wake Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uhusiano wa Tehran na Harare umo katika hatua ya kukua zaidi.

Waziri Abdollahian ameashiria mazungumzo ya hivi karibuni ya Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Zimbabwe pambizoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kwamba, azma ya viongozi wa ngazi za juu wa mataifa haya mawili ni kupanuliwa zaidi wigo wa ushirikiano baina ya nchi zao.

Viongozi wa Jamhuri ya Kiiislamu ya Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kuwa, Tehran haina mpaka katika uhusiano wake na bara la Afrika na kwamba, imekuwa ikitoa kipaumbele katika siasa zake za kigeni juu ya kuimarisha uhusiano na mataifa ya Kiafrika.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *