Mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu na vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu katika mataifa ya Ulaya hususan Ufaransa ungali unaendelea.
Katika fremu hiyo, Baraza la Utawala la Ufaransa, limeidhinisha hukumu ya kufukuzwa nchini humo Hassan Iquioussen Imam wa Swala ya Jamaa mwenye asili ya Morocco kwa tuhuma za kueneza chuki dhidi ya Mayahudi. Pamoja na hayo, hukumu hiyo imekabiliwa na malalamiko na upinzani wa akthari ya wananchi wa Ufaransa huku mamia ya watu wakikusanyika katika mji mkuu Paris kulalamikia uamuzi huo.
Waandamanaji wamelaani kile walichokitaja kuwa, chuki dhidi ya Uislamu ya viongozi wa Ufaransa. Zaidi ya misikiti 31 kaskazini mwa Ufaransa imetoa taarifa ikitangaza kumuunga mkono Sheikh Hassan Iquioussen na kumtaja kuwa mhanga wa makosa ya wazi ya tathmini ya viongozi wa serikali ya nchi hiyo ya bara Ulaya.
Pamoja na hayo, Gerald Darmanin, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Ufaransa amesema kuwa, kuidhinishwa hukumu ya kutimuliwa nchini humo kiongozi huyo wa kidini ni ushindi kwa Jamhuri ya Ufaransa.
Sheikh Hassan Iquioussen mhadhiri wa Kifaransa ni mwasisi wa Jumuiya ya Vijana Waislamu nchini Ufaransa. Mhadhiri huyo amekuwa mkosoaji mkubwa wa Mayahudi na thamani za kisekulari nchini Ufaransa. Hotuba zake zimeifanya serikali ya Ufaransa ichukue uamuzi wa pupa wa kumfukuza nchini humo.
Lucie Simon, wakili wa Sheikh Hassan Iquioussen amesema, katika miezi ijayo ataendeleza mapambano ya kutaka kutambuliwa ukiukaji wa uhuru wa kujieleza wa mteja wake na ukiukaji uliofanyika wa kumtimua nchini humo.
Hii si hatua ya kwanza kwa serikali ya ufaransa dhidi ya Waislamu. Katika miaka ya hivi karibuni, chuki dhidi ya Uislamu zimekuwa moja ya sera za serikali za Ulaya na makundi yenye kufurutu ada.
Makundi hayo yakitumia visingizio mbalimbali yamekuwa yakiushinikiza Uislamu na Waislamu sambamba kuwaandama kwa vitendo vya chuki, uadui na maudhi. Hii ni katika hakli ambayo, viongozi wa Ulaya wamekuwa wakipigia upatu suala la uhuru wa kujieleza na kutoa maoni sambamba na uhuru wa kisiasa katika bara hilo.
Licha ya madai hayo, lakini tukitupia jicho hatua zilizochukuliwa katika miaka ya hivi karibuni na tawala za Ulaya ikiwemo serikali ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa tuunaona dhahiri shahiri undumakuwili wa vigezo vya mataifa ya Magharibi kuhusiana na suala la uhuru wa kusema.
Kimsingi ni kuwa, mataifa hayo, hufungamana na nara na kaulimbiu fulani madhali fikra na matakwa yao ya kisiasa yanazingatiwa na kudhaminiwa na kutotiwa katika dhana ya kutuhumiwa. Lakini inapotokea kwamba, masuala kama usekulari, Uyahudi na ngano ya Holocaust yanapozungumziwa na kukosolewa, wakati huo mhusika huandamwa na vyombo vya mahakama na hata serikali huingilia kati na kuandaa mikakati ya kutimuliwa mhusika katika ardhi ya nchi husika.
Madola ya Magharibi yanaona kuwa kuutusi na kuuvunjia heshima Uislamu na Waislamu ni uhuru wa kusema na kutoa maoni katika mataifa hayo. Lakini anapojitokeza mtu na kukana ngano ya Holocaust au masuala mengine yanayotishia maslahi yao, wakati huo uhuru wa kusema na kutoa maoni huwekewa mipaka. Katika miaka ya hivi karibuni walimwengu wamesikia na kushuhudia misikiti mingi ikichomwa moto kwa makusudi na makundi yenye chuki na Uislamu huko Ufaransa.
Aidha wanawake Waislamu nchini Ufaransa wamekuwa wakiandamwa na madhila na vitendo mbalimbali vya maudhi kwa sababu tu ya kuvaa vazi la stara yaani hijabu. Vitendo vya unyanyasaji wanawake wanaovaa hijabu nchini Ufaransa vimeshadidi kiasi kwamba, Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, Ufaransa imekiuka hati ya kimataifa ya haki za binadamu kutokana na kuwazuia wanawake na mabinti wa Kiislamu kuvaa vazi la hijabu katika shule za nchi hiyo.
Kamati hiyo ikiihutubu serikali ya Ufaransa imeandika: Kuna haja ya kufanyiwa kazi suala la haki za binadamu hususan katika uga unaohusiana na haki za dini za waliowachache na Waislamu.
Saeed A’laa, msimamizi wa Msikiti wa Jamia wa Strasbourg nchini Ufaransa anasema: Jamii ya Waislamu barani Ulaya, inashuhudia kuongezeka hatua na vitendo vilivyo dhidi yao katika jamii sambamba na kuandamwa kwa ubaguzi jambo ambalo limezusha wasiwasi mkubwa. Hii leo tunaishi katika jamii ambayo inafuatilia utengano na badala ya kupigia debe mshikamano inazusha chuki na woga.
Filihali pia, hatua ya serikali ya Ufaransa ya kumfukuza nchini humo Hassan Iquioussen, inahesabiwa kuwa ni mfano mwingine wa wazi wa kueneza chuki dhidi ya Uislamu na kukiuka wazi na bayana uhuru wa kijamii wa jamii ya walio wachache.