Mkutano wa kihistoria kati ya Haniyah na Abbas baada ya miaka 15

Ismail Haniyah, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na Mahmoud Abbas, mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, wamekutana baada ya miaka mingi ya uhusiano wa pande mbili kukatika.

Tangu 2007, uhusiano kati ya Hamas na Mamlaka ya Ndani ya Palestina umekuwa ukikabiliwa na hitilafu kubwa, kufuatia ushindi wa Hamas katika uchaguzi wa bunge wa mwaka 2006 ambao uliiwezesha kuunda chama kikubwa katika bunge kwa kushinda viti 74. Awali harakati ya Fat’h inayoongozwa na Mahmoud Abbas ilikubali matokeo ya uchaguzi huo, lakini ikayapinga baadaye, baada ya Marekani na Ulaya kupinga matokeo hayo kwa kisingizio kuwa Hamas ni kundi la kigaidi.

Harakati ya Hamas ilipinga msimamo huo wa Fat’h na ikatangaza kwamba serikali yake ingeendelea na shughuli zake katika ukanda wa Gaza kwa sababu iliingia madarakani kwa azma ya wananchi na kupitia masanduku ya kura. Tangu wakati huo, mivutano na tofauti zilitawala katika uhusiano kati ya Hamas na Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Mshindi mkuu wa mvutano huu kati ya Hamas na Mamlaka ya Ndani ya Palestina umekuwa ni utawala wa Kizayuni wa Israel. Utawala huo umetumia fursa ya pengo hilo kuendeleza ukatili zaidi na mashinikizo ya kinyama dhidi ya Wapalestina.

Huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukiendeleza mazungumzo ya mapatano na uhusiano wa kawaida na Mamlaka ya Ndani ya Palestina, utawala huo ulichukua mkondo  wa uhasama mkubwa na vita dhidi ya Hamas na Ukanda wa Gaza. Kuhusiana na nukta hiyo, utawala wa Kizayuni uliuwekea Ukanda wa Gaza mzingiro wa pande zote wa nchi kavu, angani na baharini. Kutokana na mzingiro huo wa kinyama leo Gaza imepewa lakabu ya gereza kubwa zaidi la wazi duniani.

Mzingiro huo umepelekea watu wa Gaza wakabiliwe na hali mbaya zaidi ya kibinadamu duniani.  Aidha utawala wa Kizayuni ulianzisha vita 6 dhidi ya Wapalestina wa Ghaza katika miaka ya  2008, 2012, 2014, 2018, 2019 na 2021 na matokeo ya vita hivyo ni kuwa Wapalestina zaidi ya 3,000 waliuawa shahidi na maelfu kujeruhiwa, na makumi ya maelfu ya nyumba za makazi kuharibiwa.

Mgawanyiko kati ya Hamas na Mamlaka ya Ndani ya Palestina chini ya uongozi wa Mahmoud Abbas umekuwa ni fursa kwa utawala wa Kizayuni kuendeleza ubeberu wake dhidi ya Wapalestina. Hata wakati pande hasimu za Palestina za Hamas na Fat’h zilipokaribia kufikia mapatano, utawala wa Kizayuni ulifanya juu chini kuzuia muafaka kati ya pande hizo.

Mkutano wa hivi majuzi kati ya Haniyah na Abbas ulifanyika nchini Algeria Jumanne jioni, pembizoni mwa sherehe za miaka 60 ya uhuru wa Algeria kutoka kwa Ufaransa. Rais wa Algeria, Abdel Majid Taboun ndiye aliyewakutanisha Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Fat’h, na Ismail Haniyah, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (Hamas).

Televisheni ya Algeria wakati ikitangaza picha za mkutano huo, iliutaja mkutano kati ya pande hizo mbili kuwa wa kihistoria baada ya miaka kadhaa ya kuwa na uhusiano baridi. Harakati ya Hamas pia ilielezea mkutano huo kama wa kidugu. Algeria iliweza kuandaa mazingira ya kukutana kwa Ismail Haniyah na Mahmoud Abbas, wakati Misri ilifanya jaribio hilo mara kadhaa, lakini bila mafanikio.

Mkutano huo wa kihistoria kati ya Haniyah na Abbas umefanyika katika mkesha wa ziara ya Rais wa Marekani Joe Biden eneo la Asia Magharibi na siku chache tu baada ya kusambaratika kwa baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel chini ya Naftali Bennett. Nukta muhimu ni kwamba, mkutano kati ya Haniyah na Abbas utachukuliwa kuwa muhimu zaidi pale pande husika zitakapotatua tofauti na kuondoa vikwazo katika mwelekeo wa kupatikana maridhiano ya kitaifa na kuanzisha serikali ya umoja wa kitaifa.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *