Duru ya tatu ya mkutano wa kimataifa wa mazungumzo ya Uislamu na Uhindu iliyokuwa na anuani ya “Mchango wa Dini wa Kuishi Pamoja Katika Amani na Ustawi” umefanyika mjini New Delhi kwa kuhudhuriwa na makhatibu, shakhsia wenye vipawa na Maulamaa wa Iran na India.
Ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulioshiriki katika mkutano huo wa kimataifa umeongozwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Masuala yay Kimataifa Katika Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Washiriki wa mkutano huo mbali na kusisitiza mambo ya pamoja yaliyoko katika dini mbalimbali kwa ajili ya kufikia amani na maendeleo ya jamii ya mwanadamu, wametilia mkazo juu ya kuweko mazungumzo baina ya shakhsia wakubwa na wafuasi wa madhehebu za Kiislamu na Wahindu.
Umuhimu wa kufanyika mikutano kama hii unatokana na kuwa, ulimwengu wa leo unahitajia mno suala na amani na utulivu na bila shaka dini na Maulamaa wa dini na madhehebu zote wanaweza kuwa na mchango muhimu katika uwanja huu.
Kwa mujibu wa duru za kisiasa na kidini katika mataifa kama India ambayo ina wingi wa kaumu na madhehebu ni kuwa, kuweko mazungumzo baina ya dini mbalimbali ni jambo ambalo lina taathira chanya katika kuimarisha suala la kuishi pamoja na kwa amani watu wa dini na madhehebu tofauti. Jambo hilo kwa India lina umuhimu maradufu hasa kwa kutilia maanani kwamba, zaidi ya Waislamu milioni 200 wanaunda jamii ya wananchi wa nchi hiyo.
Soroush Amiri mweledi na mtaalamu wa mambo na aliyehitimu masomo yake nchini India anasema kuhusiana na suala hili kwamba: Katika jamii yenye kaumu na dini mbalimbali ya India, wananchi wa nchi hiyo hususan Waislamu na Wahindu daima wamekuwa wakiishi kwa amani na mchango wa Waislamu katika kusaidia kusonga mbele mipango mbalimbali ya kiviwanda na kiteknolojia nchini India ni jambo ambalo liko wazi na bayana kwa kila mtu. Pamoja na hayo baadhi ya watu wenye misimamo ya kufurutu ada wanafanya njama za kukwamisha na kuzuia mwenendo huu wa kuishi kwa amani baina ya Waislamu na Wahindu.
Hapana shaka kuwa, kufanyika makongamano ya kielimu ambayo yanahudhuriwa na Maulamaa na shakhsia wenye vipaji vya kidini wa dini mbalimbali wakiwemo Waislamu na Wahindu ni hatua inayoweza kuchangia pakubwa kuwakurubisha zaidi wafuasi wa Uislamu na Uhindu.
Hii ni kwa sababu watu ambao hawana imani na suala la mshikamano baina ya dini mbalimbali, hutumia vibaya kutokuwa na welewa watu kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la malengo yao machafu ambapo watu wenye misimamo ya kufutu ada na wanaofuatilia maslahi yao wanapatikana katika dini na katika madhehebu zote.
Hivyo basi kama walivyosisitiza shakhsia waliohutubia katika mkutano wa kimataifa wa mazungumzo ya Uislamu na Uhindu uliofanyyika huko New Delhi ni kuwa, kuimarishwa suala la mazungumzo katika uga huu ni sababu ya India na Iran kufikia katika nafasi ifaayo ulimwenguni na kusimama kidete zaidi mkabala na utumiaji mabavu na bila shaka hilo litatoa msukumo mkubwa katika kupambana na misimamo ya kufurutu ada ya kikaumu na kimadhehebu.
Ali Alai, mweledi na mchambuzi wa masauala ya India anasema: Watu wenye kufurutu wanapatikana katika dini zote, lakini nchini India kwa kuzingatia kuweko nchini humo makundi ya Kihindu kama ya Shiv Sena na Rashtriya Swayamsevak Sangh (RSS) Waislamu wa nchi hiyo wamo katika hatari zaidi ya mashambulio ya makundi hayo yenye misimamo ya kufurutu ada.
Kwa muktadha huo kadiri kutakavyokuweko na makongamano zaidi ya kuleta welewa na kuimarisha ushirikiano baina ya Maulamaa na shakhsia wenye vipawa nchini India, ni kwa kiwango hicho hicho ambapo hupelekea kupanuka wigo wa kuishi kwa amani na kuimarishwa amani na usalama wa ndani, kieneo na kimataifa.
Alaa kulli haa, wasomi na shakhsia wenye vipawa walioshiriki katika mkutano wa kimataifa wa mazungumzo baina ya Uislamu na Uhindu uliofanyika huko New Delhi sanjari na kuashiria athari nzuri za mazungumzo baina ya dini mbalimbali, wametoa mwito wa kudumishwa makongamano kama haya kwa minajili ya kuleta zaidi hali ya kukaribiana na urafiki baina ya Waislamu na Wahindu.
Suala hili linapata umuhimu zaidi hasa kwa kutilia maanani kwamba, aghalabu ya wananchi wa India wanaheshimu Uislamu na Waislamu na hata baadhi yao hushiriki kumbukumbu ya Ashura. Waislamu nao kwa upande wake siku zote wamekuwa wakiheshimu itikadi za dini ya Wahindu.
Anga hiyo inayotawala nchini India imeyatia wasiwasi mkubwa makundi yenye misimamo ya kufurutu ada na vilevile vibaraka kutoka nje wenye taathira kama Wazayuni. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana daima wamekuwa wakichukua hatua chafu zenye lengo la kuzusha mifarakano baina ya wafuasi wa dini tofauti nchini humo. Hii ni katika hali ambayo, lengo la dini zote ni kuleta amani na utulivu sambamba na kuandaa mazingira na anga ya kuishi kwa usalama na amani baina ya wafuasi wa dini tofauti.
Pamoja na hayo yote lakini hatupaswi kufumbia macho ukweli huu kwamba, serikali iliyoko madarakani nchini India imekuwa na utendaji ulio dhidi ya Waislamu.
Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi imewawekea vikwazo na vizuizi vingi Waislamu wa nchi hiyo. Siasa na sera za serikali ya India za kukandamiza na kukiuka haki za Waislamu zimepelekea Wahindu wenye itikadi na misimamo mikali, wanaoungwa mkono na chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) chenye misimamo ya kufurutu mpaka ya utaifa wa kihindu, kuchukua hatua mbalimbali za kuwashambulia na hata kuwaua Waislamu wa nchi hiyo.