Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA amekiri kuwa nchi hiyo haina tena mamlaka ya juu yasiyopingika katika siasa za ulimwengu.
William Burns ameyasema hayo katika andiko lake lililochapishwa katika toleo la jana la gazeti la Foreign Affairs na kueleza kwamba, kuongezeka kwa nguvu za kijeshi na kiuchumi za China, nia ya Russia ya kutumia nguvu za kijeshi nchini Ukraine, na kuongezeka kwa idadi ya madola ya kikanda yanayofuata sera huru za kigeni, yote hayo yamesababisha “ulimwengu wa ushindani mkali wa kimkakati ambapo Marekani haijifaragui tena kwa kuwa na mamlaka makuu yasiyopingwa”.
Burns amebainisha katika makala yake hiyo kwamba, sambamba na mamlaka ya Marekani kukabiliwa na changamoto nyingi kuliko wakati wowote ule tangu kumalizika kwa Vita Baridi, CIA imeongeza juhudi zake za kuandaa na kuongeza maajenti wa kukabiliana na Russia na kufungua “kituo kipya cha majukumu” maalumu kwa ajili ya China.
Sehemu kubwa ya makala hiyo inatoa hoja ya kuendelezwa misaada ya kijeshi kwa Ukraine, na kusisitiza kama walivyosikika maafisa wengine wa Washington kwamba, kukatishwa msaada wa silaha za Magharibi kwa Kiev kutafikisha ujumbe kwa China wa “kutojali Marekani” na hivyo kumtia moyo Rais Xi Jinping wa kushambulia Taiwan.
Mkuu huyo wa CIA ameendelea kueleza kwamba, ingawa Russia inaweza kuwa changamoto ya haraka zaidi, China ndilo tishio kubwa la muda mrefu kwa Marekani.
Itakumbukwa kuwa, CIA ilipata pigo kubwa katika uwezo wake wa kukusanya taarifa za kijasusi mwaka 2010, wakati mamlaka ya China ilipoanza kuwatambua, kuwakamata na kuripotiwa kuwanyonga maajenti wa CIA nchini humo. Uchunguzi uliofanywa na gazeti la New York Times ulisema idadi ya majasusi waliouawa au kufungwa ni 20, huku jarida la Foreign Policy likidai kuwa maajenti 30 waliuawa nchini China kati ya 2010 na 2012.