Mkuu wa Hamas: Uhalifu wa Israel dhidi ya mfungwa wa Kipalestina aliyekuwa anaugua saratani hautapita bila kuadhibiwa

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Palestina, Hamas, amelaani kifo cha mfungwa wa Kipalestina aliyekuwa anaugua kansa katika jela za Israel na kusema kuwa jinai za utawala huo hazitapita bila kuadhibiwa.

Ismail Haniyeh aliyasema hayo katika taarifa siku ya Jumanne, baada ya Nasser Abu Hamid, ambaye alikuwa anasumbuliwa na hali ya kiafya ya kutishia maisha katika mapafu yake akiwa kizuizini Israel, kutangazwa kuaga dunia na Tume ya Wafungwa wa Palestina mapema hapo jana.

Ismail Hania ametuma salamu za rambirambi za dhati kufuatia kifo cha Abu Hamid kwa mama yake na ndugu zake waliowekwa kizuizini katika jela za utawala haramu wa Israel na kusisitiza dhamira ya harakati hiyo ya kuwakomboa wafungwa wote wa Kipalestina wanaoteseka katika jela za utawala huo wa kibaguzi.

Abu Hamid alitangazwa kufariki dunia Jumanne asubuhi katika Kituo cha Matibabu cha Shamir cha Israeli, kilichoko kilomita 15 (maili 9.3) kusini mashariki mwa Tel Aviv.

Alihamishwa kutoka Hospitali ya Gereza ya Ramla hadi kituo hicho cha matibabu Jumatatu alasiri baada ya hali yake ya afya kuzorota na kuingia kwenye koma.

Abu Hamid aligunduliwa kuwa na saratani mnamo Agosti 2021.

Mfungwa huyo wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 50 alikuwa akikabiliwa na hali ngumu ya afya huku magereza ya Israel (IPS) yakimnyima huduma muhimu za matibabu.

Septemba iliyopita, madaktari wa Israel walitoa ripoti ya matibabu wakipendekeza aachiliwe huru, wakisema saratani yake ya mapafu ilikuwa imefikia hatua isiyoweza kutibika.

Hivi karibuni familia yake ilikuwa imetoa wito kwa mashirika ya kimataifa kuchukua hatua za dharura na madhubuti ili kuokoa maisha yake.

Wakati huo huo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Palestina, Riyad al-Maliki, amesema utawala wa Israel unahusika moja kwa moja na kifo cha Abu Hamid, na kusisitiza kuwa kesi yake itawasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Maliki pia ameishutumu jamii ya kimataifa kwa kushindwa kushughulikia suala la Abu Hamid kwa wakati unaofaa, akisema sio tu kwamba ni mwathirika wa ukandamizaji wa utawala ghasibu wa Israel, bali pia ni mwathirika wa undumakuwili wa kimataifa.

Aidha ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuushinikiza utawala wa kibaguzi wa Israel ukabidhi mwili wa mfungwa huyo wa Kipalestina kwa familia yake, ili imzike haraka iwezekanavyo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *