Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia amesema: Maajinabi hawawezi kusimamisha sekta ya nyuklia ya Iran.
Seyed Hossein Feqhi, Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia ya Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ameeleza katika mkutano na waandishi wa habari kwa mnasaba wa Wiki ya Utafiti: “tumeshavuka hatua ya sababu ya nje kuweza kuisimamisha Iran katika sekta ya nyuklia kwa kisingizio chochote kile”.
Kwa mujibu wa shirika la habari la ISNA, Feqhi ameongeza kwamba, kwa mara ya kwanza Taasisi ya Utafiti wa Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia imekabidhiwa jukumu la kujenga kinu cha utafiti wa nyuklia nchini na kazi hiyo tayari imeshaanza.
Feqhi amefafanua kwa kusema: “suala hili ni muhimu sana kwa sababu linaonyesha kwamba katika baadhi ya nyanja tumeshavuka hatua ya utafiti na kuingia kwenye hatua ya uundaji na utumiaji, na bila shaka linafanyika hilo kwa msaada wa makampuni ya kitaalamu ambayo yanafanya kazi katika nyuga hizi”.
Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia ya Shirika la Nishati ya Atomiki amebainisha pia kwamba, kustawisha uhusiano wa kimataifa na ushirikiano mpana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA katika uga wa utafiti ni ajenda inayofanyiwa kazi na taasisi hiyo, Shirika la Nishati ya Atomiki na serikali.
Kuhusu madai ya baadhi ya nchi ikiwemo Marekani kwamba Iran inataka kuwa na silaha za nyuklia, Feqhi amesema: “Huu ni uwongo mkubwa wenye dhamira ya kusimamisha sekta ya nyuklia ya Iran; hakuna dalili yoyote ya kitaalamu ya kuituhumu Iran kuwa inataka kutengeneza silaha za nyuklia wala hakuna mtafiti yeyote pia anayethibitisha dai hili”.
Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia ameeleza pia kuwa, hatua zote za Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran zinachukuliwa kwa mujibu wa itifaki zinazokubalika kimataifa.