Polisi wa Nigeria wamemuua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine kadhaa katika shambulizi lililofanywa dhidi ya waandamanaji wa Siku ya Al-Quds Duniani huko Zaria, Jimbo la Kaduna.
Takriban mtu mmoja aliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati polisi walipowafyatulia risasi wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) wakati wa maandamano ya Siku ya Dunia ya Al-Quds huko Zaria, Jimbo la Kaduna, kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Al-Ahd ya Lebanon.
Kwa mujibu wa Al-Ahd, baadhi ya miji ya Nigeria jana (Ijumaa) katika siku ya mwisho ya Ramadhani ilishuhudia maandamano makubwa ya kulaani mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya Jerusalem inayokaliwa kwa mabavu na kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Jerusalem.
Maandamano hayo yalifanyika kwa mwaliko wa Sheikh Ibrahim Al-Zakzaki, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
Waandamanaji hao wamelaani mashambulizi ya mara kwa mara ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa na jinai zake dhidi ya wananchi wa Palestina.Waandamanaji hao aidha wameutaka Umma wa Kiislamu kukabiliana na Wazayuni.
Mapema Sheikh Al-Zakzaki alitoa wito kwa wafuasi na waungaji mkono wake kufanya kila wawezalo kuadhimisha Siku ya Quds Duniani mwaka huu tofauti na miaka ya nyuma.
Mtu aliyeshuhudia tukio hilo aliliambia gazeti la SaharaReporters kwamba wanachama wa Harakati ya Kiislamu walikuwa wakienda kwa utulivu wakati polisi walipofika ghafla na kuwafyatulia risasi.
Alibainisha kuwa mmoja wa waandamanaji hao alifariki kutokana na kuchomwa moto na polisi.Aliongeza kuwa wengine kadhaa pia walipigwa risasi na kwa sasa wamelazwa hospitalini.