Mmoja wa wakurugenzi wa Twitter ahukumiwa kifungo kwa kuifanyia ujasusi Saudi Arabia

Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Marekani imepelekea kuhukumiwa mmoja wa wakurugenzi wa zamani wa mtandao wa kijamii wa Twitter kifungo cha miaka mitatu na nusu jela kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa manufaa ya Saudi Arabia.

Wawakilishi wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka huyo walikuwa wameomba kifungo cha miaka saba jela dhidi ya Abu Amu kwa hoja kwamba walitaka kifungo kiwe kikali ili kutoa ujumbe wa kuwazuia wengine katika sekta ya teknolojia na mitandao ya kijamii kuuza data na habari za watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Mahakama ilimpata kuwa na hatia Ahmed Abu Amu mwezi Agosti baada ya kusikilizwa kesi yake katika mahakama ya shirikisho huko San Francisco. Wakati huo, alihukumiwa miaka 10 jela kwa shtaka moja na miaka 20 kwa mashtaka mengine kadhaa.

Wawakilishi wa mwendesha mashtaka pia walitangaza kuwa mkurugenzi huyo huyo wa zamani wa Twitter alipokea rushwa kutoka kwa maafisa wa Saudi mwaka 2014, ikiwa ni pamoja na saa ya thamani ya dola 42,000 na kuhamishiwa dola 100,000 katika akaunti yake binafsi ya benki.

Katika kesi hiyo mawakili wa Ahmed Abu Amu walimwomba hakimu wa mahakama ampe kifungo cha kusalia nyumbani kwake huko Seattle kwa hoja kuwa alikuwa na matatizo ya kiafya.

Akiwa anafanya kazi kwenye shirika la Twitter, Ahmed Abu Amu alisimamia kitengo cha uhusiano na waandishi wa habari na watu mashuhuri katika eneo la Asia Magharibi na Afrika Kaskazini. Pia amepatikana na hatia ya kuhamisha taarifa nyeti kutoka mifumo ya shirika hilo ili kuwasaidia watawala wa Saudi kuwatambua na kuwakamata watumiaji wanaotafutwa na utawala wa Riyadh.

Ikumbukwe kuwa mwezi Julai iliyopita, gazeti la Marekani la New York Times lilifichua undani wa tuhuma zilizokuwa zinamkabili Ahmed Abu Amu katika kuifanyia ujasusi Saudi Arabia. Aidha, kwa mujibu wa Idara ya Sheria ya Marekani, mkurugenzi huyo wa zamani wa Twitter pia alihusika katika kuwasaidia watumiaji kupata baji ya “Twitter Blue.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *