Baraza Kuu la Muungano wa Falme za Kiarabu limemteua Mohammed bin Zayed Aal Nahyan kuwa rais mpya wa nchi hiyo.
Televisheni ya al Jazeera imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, uteuzi huo umekuja baada ya kufariki dunia rais wa nchi hiyo, Sheikh Khalifa bin Zayed Aal Nahyan. Khalifa bin Zayed alifariki dunia jana Ijumaa akiwa na umri wa miaka 73.
Khalifa bin Zayed Aal Nahyan ndiye aliyekuwa mtoto mkubwa wa kiume wa Zayed bin Sultan Aal Nayhan, mwasisi wa Muungano wa Falme za Kiarabu na ndiye aliyekuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Abu Dhabi kabla ya kutwaa madaraka kamili baada ya kufariki dunia baba yake.
Hivi sasa Mohammed bin Zayed Aal Nahyan ametwaa madaraka hayo mara baada ya kufariki dunia kaka yake na kilichofanyika hivi sasa ni kukamilisha tu taratibu za kifalme za kumtangaza rasmi kuwa rais wa Imarati.
Khalifa bin Zayed alikuwa rais wa pili wa Muungano wa Falme za Kirabu tangu ilipoundwa nchi hiyo tarehe 2 Disemba 1971. Alikuwa mtawala wa 15 wa Abu Dhabi.
Khalifa bin Zayed, alikuwa akionekana kwa nadra hadharani tangu alipopata maradhi ya kiharusi mwaka 2014, huku ndugu yake, mrithi wa ufalme wa Abu Dhabi Mohammed bin Zayed, maarufu kama MBZ akionekana kuwa ndiye mtawala halisi na mpitishaji mkuu wa maamuzi katika sera kuu za nje, ikiwemo hatua ya Muungano huo wa Falme za Kiarabu kujiunga katika vita vinavyoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen na kushiriki katika mpango wa kuiwekea vikwazo nchi ya Kiarabu ya Qatar katika miaka ya karibuni.