Rais wa zamani wa Tunisia amewaonya viongozi wa Saudi Arabia kwa hatua yao ya kutekeleza adhabu ya kifo kwa watu 81 kwa siku moja na kuwaambia wajiandae kwa madhara ya hatua yao hiyo.
Siku ya Jumamosi, wizara ya mambo ya ndani ya Saudia iitekeleza adhabu ya kifo kwa watu 81 ikidai kuwa watu hao wamefanya jinai zisizosameheka.
Rais wa zamani wa Tunisia, Moncef Marzouki amelaani kuuliwa kwa umati watu hao 81 katika siku moja na kusema kuwa utawala wa ukoo wa Aal Saudi umefanya jinai hiyo katika hali ambayo dunia hivi sasa imeshughulishwa na vita vya Ukraine.
Ni vyema tukumbushe hapa kwamba, 41 kati ya watu hao 81 waliotekelezewa adhabu ya kifo kwa siku moja huko Saudia, walikuwa ni vijana wa Kishia wa eneo la Qatif la nchi hiyo. Wengi wa vijana hao walikamatwa na serikali ya Saudi Arabia kwa madai tofauti na kusukumwa korokoroni.
Katika kujaribu kuhalalisha jinai hiyo, wizara ya mambo ya ndani ya Saudi Arabia imedai kuwa watu hao 81 ni watu waliopotoka, walikuwa wakimfuata shetani na fikra potofu na walikuwa wakitumiwa na wageni kufanya vitendo vilivyo dhidi ya watawala.
Kwa upande wake, Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Jumatatu alilaumu vikali misimamo ya nyuso mbili ya nchi na mashirika yanayodai kupigania haki za binadamu duniani na kusema kuwa, kimya cha nchi na mashirika hayo kuhusu mauaji ya umati ya watu 81 yaliyofanywa na viongozi wa Saudia, lazima kilaaniwe.
Alisema, misimao hiyo ya nyuso mbili ya nchi za Magharibi imeonesha wazi kuwa lengo la nchi hizo ni kutumia kisiasa tu suala la haki za binadamu ili kutimiza tamaa zao za kiistikbari na kuzishinikiza nchi huru ulimwenguni.