Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ukraine mapema leo Ijumaa amesema kuwa moto mkubwa umetokea katika kituo kikubwa zaidi cha nyuklia cha nchi hiyo cha Zaporizhzhia.
Dmytro Kuleba amedai kuwa moto huo umetokana na mashambulizi ya Jeshi la Russia dhidi ya kituo hicho.
Zaporizhzhia ndicho kituo kikubwa zaidi cha nishati ya nyuklia nchini Ukraine na pia barani Ulaya.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ukraine amedai kuwa iwapo kituo hicho cha nyuklia kitalipuka kisababisha mlipuko mkubwa zaidi wa nyuklia wenye nguvu mara kumi zaidi ya ya mlipuko wa kituo cha nyuklia cha Chernobyl.
Mlipuko wa kituo cha nyuklia cha Chernobyl ulitokea tarehe 26 Aprili mwaka 1986 katika kinu nambari 4 cha kituo hicho na kusababisha vifo vya makumi ya watu.
Kiwanda cha nyuklia cha Chernobyl kwa sasa kiko chini ya udhibiti wa Russia.
Serikali ya Ukraine imesisitiza kuwa kituo cha nyuklia cha Zaporizhzhia kiko salama.
Jana Alkhamisi Jeshi la Russia lilitangaza kuwa limeuteka mji wa Bahari Nyeusi wa Kherson wa nchini Ukraine huku likiendelea kusonga mbele katika miji mingine ya nchi hiyo ya Ulaya Mashariki.
Rais Vladimir Putin wa Russia anasema kuwa, lengo lake si kukalia kwa mabavu ardhi ya Ukraine, bali ni kuipokonya silaha ili kulinda usalama wa kitaifa wa Russia.