Msafara wa baharini wa Lebanon waelekea mpaka wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu kulinda maliasili zake

Msafara wa majini wa Lebanon umeanza safari yake ya kuelekea mpaka wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) kwa lengo la kulinda utajiri wa nchi hiyo wa maliasili za mafuta na gesi dhidi ya uporaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, msafara wa majini wa Lebanon ambao uliandaliwa siku chache zilizopita kwa ajili ya kutetea na kulinda haki za baharini za nchi hiyo dhidi ya uvamizi na uchokozi wa utawala wa Kizayuni, leo umeondoka katika bandari za kaskazini mwa Lebanon ikiwemo ya Tripoli kuelekea eneo la Al Naqourah upande wa kusini, ambao uko kwenye mpaka wa pamoja na Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Faisal Derniqah, mratibu wa kampeni ya kiraia ya kulinda utajiri wa taifa wa Lebanon amesema, “harakati hizi zinalenga kufikisha ujumbe kwa utawala wa Kizayuni kwamba utajiri wa taifa wa Lebanon ni mstari mwekundu kwetu sisi, na wananchi wa Lebanon hawatafumbia macho hata tone moja la gesi na mafuta yao yaliyoko baharini.”
Abdul Nasser al-Masri, Mkuu wa Kamati ya Wananchi ya Kampeni ya Kutetea Utajiri wa Kitaifa wa Lebanon, naye pia amesema kuhusiana na suala hilo kwamba, boti zilizotoka Tripoli zinaungana na msafara wa baharini kutoka bandari za kaskazini mwa Lebanon hadi kufika mpakani mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Al-Masri amesisitiza kuwa, kinachoilinda Lebanon ni Pembetatu za Dhahabu zinazojumuisha jeshi, wananchi na muqawama, ambavyo ndivyo vinavyodhamini haki za Walebanon wote.

Mzozo kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Lebanon kuhusu mipaka ya bahari ya pande hizo mbili umeongezeka, huku Wazayuni wakiwa wanavikodolea macho visima vya Qana vyenye utajiri mkubwa wa gesi ambayo ni mali ya Lebanon.
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa, theluthi mbili ya visima hivyo ziko katika Kitalu nambari tisa cha Lebanon na theluthi moja ya mwisho iko chini kabisa ya mstari wa 23, yaani, katika eneo linalozozaniwa.
Hivi karibuni na baada ya kukiuka mpaka wa baharini wa Lebanon, utawala wa Kizayuni uliweka jukwaa la gesi katika Bahari ya Mediterania.
Israel iliweka jukwaa hilo la gesi katika eneo la Karish ili kulitumia kwa shughuli za uchunguzi na uchimbaji gesi. Hata hivyo hatua yake hiyo ilikabiliwa na majibu makali ya viongozi wa Lebanon.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *