Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ameeleza kuwa mapambano ya kulinda na kuutetea msikiti wa al Aqsa na mateka wa Kipalestina yatakuwa ya aina yake na kusisitiza kuwa utawala wa Kizayuni unawajibika kubeba dhima ya matokeo ya hatua za kichochezi za Ben Gvir.
Abdullatif al Qanui Msemaji wa Hamas amesema akihutubia hadhara akiwa mbele ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Ghaza kuwa kadhia ya mateka shujaa wa Kipalestina walioko katika jela za utawala wa Kizayuni ni suala kuu linalopewa uzito na kipaumbele na harakati ya Hamas. Hamas imesema kuwa, viongozi wa Palestina wako tayari kuwaunga mkono na kuwasaidia mateka wake katika mapambano na mashinikizo yoyote.
Al Qanui ameeleza kuwa, Hamas na watoto wote wa taifa la Palestina na mapambano yao suku na mchana wanafuatilia nyenendo za utawala ghasibu mkabala wa mateka wa Kipalestina. “Tunautahadharisha utawala ghasibu kwamba mapambano ya kuulinda msikiti wa al Aqsa na mateka wa Kipalestina yatakuwa tofauti na mifano na matukio yote yaliyopita,” amesema Msemaji wa Hamas.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake huko Ghaza, Msemaji wa Hamas amesisitiza kuwa Tev Aviv ndiyo itakayobeba dhima na kuwajibika na taathira hatari za matamshi na vitendo vya kichochezi vya Itamar Ben Gvir Waziri mwenye misimamo ya kufurutu ada wa utawala wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al Aqsa na mateka wa Kipalestina. Taathira hizo zitaliathiri eneo zima, amesema al Qanui.
Hivi Karibuni Ben Gvir Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni akiwa katika siku za awali akihudumu katika nafasi hiyo huku akiambatana na kundi la Wazayuni kadhaa wakisindikizwa na wanajeshi wa utawala huo haramu walivamia msikiti wa al Aqsa katika hatua ya kichochezi; kitendo kilicholaaniwa pakubwa na Waislamu na nchi mbalimbali za Kiislamu duniani.