Shirika lisilo la kiserikali la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limetangaza kuwa, limeanza tena kutoa huduma katika kambi ya wakimbizi ya mji wa El Fasher wa Darfur Kaskazini huko magharibi mwa Sudan kutokana na watu katika kambi hiyo kukumbwa na njaa kali na magonjwa ya kuambukiza.
Kundi hilo limesema hayo katika mtandao wa kijamii wa X kwa kuandika: “Baada ya kupita siku 60, tumeanzisha tena mpango wetu kamili wa lishe kwa wagonjwa kwani hatimaye tumepokea masanduku 2,433 ya Vyakula vya Tiba Vilivyo tayari Kutumika (RUTFs) na vifaa vingine vya matibabu.”
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema: “Kiwango hiki kinatosha kwa wiki tano tu. Tulipungukiwa na chakula cha matibabu mwezi Septemba hivyo tulilazimika kuacha kutoa huduma hizo za kuokoa maisha ya watoto 5,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano ambao wako katikati ya janga kubwa la njaa.”
Mapema mwezi Agosti, MSF iliripoti kuwa imelazimika kupunguza kuhudumia watoto wenye utapiamlo katika kambi ya Zamzam ambayo ni moja ya kambi kubwa zaidi za wakimbizi huko Darfur, Sudan, kutokana na ukwamishaji wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Sudan imeharibiwa vibaya na mgogoro wa uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF tangu katikati ya mwezi Aprili 2023.
Tangu tarehe 10 Mei mwaka huu, mapigano makali yanaendelea kushuhudiwa katika mji wa El Fasher, makao makuu wa jimbo la Darfur Kaskazini la magharibi mwa Sudan baina ya makundi hayo mawili huku zaidi ya watu 750,000 wakiwa kwenye janga la uhaba mkubwa wa chakula.