Mtangazaji wa TV wa Ujerumani afutwa kazi kwa kuiunga mkono Palestina

Matondo Castlo mwendeshaji wa kipindi cha watoto katika kanali ya televisheni ya KiKA ya Ujerumani amefutwa kazi baada ya kushiriki maandamano ya amani katika mji wa Bait Dajan huko mashariki mwa mji wa Nablus. Ametuhumiwa kuwa ana chuki dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Matondo Castlo alituma ujumbe kwenye akaunti yake ya Instagram kwamba alifutwa kazi wiki hii na kanali ya televisheni ya KiKA ambayo ni kituo cha televisheni cha watoto nchini Ujerumani kwa hatua yake ya kushiriki maandamano katika mji wa Beit Dajan karibu na Nablus huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel mwezi Agosti mwaka huu.

Castlo ameeleza kuwa, maandamano hayo yalikuwa ya amani na lengo lake lilikuwa ni kulalamikia hatua za walowezi wa Kizayuni na wanajeshi wa utawala ghasibu unaoikalia Quds kwa mabavu za kuzipora ardhi za Wapalestina. Matondo Castlo ameongeza kuwa: hakuwa na nia ya kutoa taarifa ya kisiasa na hata hakuchukua msimamo wowote dhidi ya Israel.

Wakati huo huo magazeti ya Ujerumani yameandika taarifa hii kuhusu kushiriki mtangazaji huyo wa televisheni ya KiKA katika maandamano ya wanaoiunga mkono Palestina na kuchapisha makala chini ya anwani “Tamasha la Uchupaji Mipaka” kwamba: Mtangazaji wa KiKA ameandamana bega kwa bega na wapinzani wa Israel ili kwa njia hiyo kujaribu kuamsha fikra za walio wengi dhidi ya Costlo.

Televisheni ya KiKA pia imetangaza kuwa imeamua kutoendelea kufanya kazi na Castlo hadi masuala yote kuhusu kadhia hiyo yatakapopatiwa ufafanuzi. Hii si mara ya kwanza kwa mwendesha kipindi cha televisheni nchini Ujerumani kufukuzwa kazi kwa kuwaunga mkono Wapalestina.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *