Mtoto wa miaka 6 ampiga risasi mwalimu wake kwa ‘makusudi’ Marekani

Mtoto wa miaka sita huko nchini Marekani ametiwa mbaroni baada ya kumpiga risasi na kumjeruhi vibaya mwalimu wake katika mji wa Newport News, jimboni Virginia.

Mkuu wa Polisi katika mji wa Newport News, Steve Drew amethibitisha habari ya kutokea tukio hilo hapo jana Ijumaa katika shule ya msingi ya Richneck, katika mji wa Newport News, jimboni Virginia, kusini mashariki ma Marekani.

Drew amesema mtoto huyo mvulana wa miaka sita alimpiga risasi mwalimu wa kike mwenye umri wa maika 30 ambaye jina lake halikutajwa, baada ya wawili hao kuzozana na kuhitilifiana wakiwa darasani. Polisi haijaeleza alikotoa bastola mtoto huyo wa miaka sita, au malumbano baina yake na mwalimu wake yalihusu nini.

Mwanafunzi mmoja aliyekuwa darasani wakati wa tukio hilo ameliambia gazeti la Newport News kuwa, “Mwalimu alipigwa risasi tumboni kwa makusudi, kisha akadondoka chini.”

Machi mwaka jana, tukio jingine la kusikitisha lilitokea nchini Marekani baada ya mtoto wa miaka mitatu kumuua mama yake kwa kumpiga risasi katika mji wa Dolton

Maelfu ya raia wa Marekani huuawa kila mwaka katika matukio ya mashambulizi ya silaha za moto katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. Vitendo vya ukatili wa silaha za moto nchini Marekani vimegeuka kuwa moja ya matatizo makubwa na sugu katika jamii ya Marekani, huku makundi ya haki za raia yakitaka kuwepo sheria za kubana umiliki wa bunduki mikononi mwa raia.

Hivi karibuni, mtandao wa Hifadhi ya Ukatili wa Silaha nchini Marekani uliripoti kwamba, mwaka uliomalizika wa 2022, zaidi ya watoto 6,000 wa nchi hiyo waliuawa au kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na vurugu za kutumia silaha, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika kipindi cha miaka 9 iliyopita.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *