Mtoto wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amesema kwamba kundi la waasi la M23, linalopigana vita na jeshi la serikali ya Kinshasa, lina haki ya kufanya hivyo.
Muhoozi ameandika katika ujumbe wa twitter akisema kwamba “ni hatari sana kwa mtu yeyote kupiga vita ndugu zetu. Sio magaidi, bali wanapigania haki za Watutsi wanaoishi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.”
Msimamo wa Jenerali Muhoozi ni tofauti na msimamo wa serikali ya Uganda ambayo imelazimika kutoa taarifa kupitia kwa msemaji wake Ofwono Opondo, kufuatia ripoti kwamba Uganda inaunga mkono wapiganaji wa M23.
Opondo alisema wiki hii kwamba “Uganda haiungi mkono kundi la waasi la M23” na kwamba “Uganda ina husiano mzuri sana na serikali ya Kinshasa katika kupigana na kundi la waasi la Allied democratic movement ADF.”
Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo waliandamana mapema wiki hii, hadi kwenye mpaka wa DRC na Rwanda, wakidai kwamba Uganda na Rwanda zinaunga mkono waasi wa M23, na kutaka mpaka kati ya DRC na nchi hizo mbili kufungwa.
Baadhi wa bunge na maseneta wa DRC vile vile walitaka DRC kufunga mpaka wake na Uganda, wakisema kwamba Uganda inaunga mkono makundi ya wapiganaji wanaoisumbua serikali ya Congo.
Mapema jana Jumapili, ndege za vita za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ziliwasili mjini Goma. Japo serikali haijatoa taarifa yoyote kuhusu ndege zake za kurusha makombora na zile zisizo na rubani kuwasili Goma, vyombo vya habari vya DRC vimeripoti kwamba jeshi la Kinshasa lipo tayari kuanza mashambulizi makali dhidi ya makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo. Usafiri wa ndege za kawaida umesitishwa kwa saa kadhaa wakati ndege hizo za kijeshi zilikuwa zinaingia Goma.