Muqtada Sadr, Kiongozi wa Harakati ya Sadr ya Iraq ametangaza kujiuzulu harakati na shughuli zote za kisiasa.
Uamuzi huo ambao haukutarajiwa hasa katika kipindi hiki cha mkwamo wa kisiasa nchini Iraq ambao mrengo wake unatuhumiwa kuhusika, ameuchukua baada ya taarifa muhimu iliyotolewa na Ayatullah Sayyid Kadhim Hairi.
Sayyid Muqtada Sadr ametangaza kuwa, hakuna wakati ambao alidai uongozi au Umarjaa na kwamba, kuanzia leo anatangaza rasmi kuachana na harakati na shughuli zote za kisiasa.
Ayatullah Hairi Marjaa Taqlidi wa Kishia ambaye anatambuliwa na wengi kama muungaji mkono wa Muqtada Sadr na harakati yake, leo ametangaza kujivua jukumu la Umarjaa kutokana na sababu za maradhi na uzee.
Katika taarifa yake, Ayatullah Hairi alimhutubu Muqtada Sadr Kiongozi wa Harakati ya Sadr ya Iraq kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kukosoa fitina na ufarakishanaji wananchi wa Iraq kwa kutumia jina la mashahidi Sadr.
Akiendelea kubainisha uamuzi wake wa kuachia ngazi shughuli za kisiasa, Muqtada Sadr ametangaza kufunga ofisi na asasi zote zenye mfungamano na Harakati ya Sadr isipokuwa asasi mbili za kiutamaduni za Sadr.
Hii si mara ya kwanza kwa Muqtada Sadr, Kiongozi wa Harakati ya Sadr kutangaza kujiuzulu shughuli za kisiasa kwani miaka 9 iliyopita alitangaza uamuzi kama huo lakini baadaye akarejea katika ulingo wa siasa.