Muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia umepora mapipa laki nne ya mafuta ya Yemen

Meli moja ya mafuta ya kigeni inayomilikiwa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia imeondoka katika mkoa wa Shabwah, kusini mashariki ya Yemen baada ya kupora mapipa laki nne ya mafuta ghafi ya nchi hiyo.

Duru moja ya Yemen imesema, meli hiyo iliondoka Muungano wa Falme za Kiarabu, Imarati siku kadhaa zilizopita na kuingia bandari ya Rudhum mkoani Shabwah na kwamba baada ya kupora mapipa laki nne ya mafuta ghafi imeondoka bandarini hapo leo.

Kwa mujibu wa duru hiyo, mafuta hayo yaliyoibiwa na muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia yana thamani ya dola milioni 43 na laki sita na 40, sawa na riyali bilioni 49 za Yemen.

Hayo yanajiri wakati mnamo wiki mbili zilizopita pia meli nyingine moja ilipora mapipa zaidi ya milioni mbili ya mafuta ghafi ya Yemen katika bandari ya Ash-Shihr huko Hadhramaut.

Raia wa Yemen walioko Shabwa na katika mikoa mingine ya nchi hiyo wanataabika kutokana na uhaba wa mafuta wakati maelfu ya tani za mafuta ghafi ya nchi hiyo zinaendelea kuporwa.

Mnamo mwaka jana, Muin Abdulmalik, waziri mkuu wa Yemen aliyejitangaza mwenyewe na aliye na mfungamano na muungano vamizi wa Saudia na Imarati aliidhinisha makubaliano yanayouhalalishia utawala wa Riyadh kupora rasmi mafuta ya Yemen.

Hatua hiyo ni sehemu ya ufanikishaji wa njama ya Saudi Arabia ya kupora maliasili muhimu za maeneo ya kusini na mashariki ya Yemen.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *