Muungano vamizi unaoongozwa na Saudia na Imarati unaendelea kufanya jinai dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa nchi ya Kiarabu ya Yemen.
Tangu mwezi Machi 2015 hadi hivi sasa, kila siku wananchi wasio na hatia wa Yemen wanamiminiwa mabomu na makombora na wavamizi wa nchi yao wanaoongozwa na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu mbali na nchi yao kuzingirwa kila upande, angani, ardhini na baharini.
Muqawama na kusimama kidete wananchi Waislamu wa Yemen kumezidi kuwatia hamaki wavamizi wa nchi hiyo na wiki za hivi karibuni wamezidisha mno mashambulizi yao katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Televisheni ya al Masirah imeripoti kuwa, mapema leo asubuhi, madola vamizi ya Imarati na Saudia yamendelea kushambulia maeneo ya raia katika mji mkuu wa Yemen, Sana’a.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, maeneo mengine ya Yemen yakiwemo ya mkoa wa Hadhramaut yamekumbwa na mashambulio ya ndege za wavamizi.
Kabla ya hapo pia, vyombo mbalimbali vya habari vilikuwa vimeripoti kuwa, jana Jumanne, maeneo ya makazi ya raia katika mikoa ya Hajjah, Ma’rib, Saada, Sana’a, Taiz n.k, ilishambuliwa vibaya na ndege za kivita za wavamizi hao.
Brigedia Jenerali Yahya Saree, Msemaji wa Majeshi ya Yemen amesema, jinai za wavamizi za kushambulia taasisi na maeneo ya raia huko Yemen hazitoachwa vivi hivi bila ya majibu makali ya kulipiza kisasi.