Huku yakitangaza taathira na madhara ya Azimio la Balfour ambalo lilliunga mkono rasmi kuanzishwa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Palestina, makundi ya mapambano ya Palestina yamesisitiza juu ya kuendeleza mapambano dhidi ya utawala huo.
Faraan: Tarehe 2 Novemba 1917 Arthur James Balfour ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza alitangaza na kumtumia azimio hilo Baron Walter Rothschild, kiongozi wa jamii ya Mayahudi nchini Uingereza ambaye pia alikuwa mbunge wa nchi hiyo. Azimio hilo lilitoa kibali cha kuasisiwa kidhalimu utawala haramu wa Israel katika ardhi za Wapalestina. Aziomio hilo ndio ulikuwa msingi wa kubuniwa rasmi utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi zilizoghusubiwa za Wapalestina mwaka 1948.
Makundi ya mapambano ya Palestina yanaamini kuwa msingi wa jinai na kughusubiwa ardhi zao na Israel unafungamana na Azimio la Balfour na hivyo kusisitiza kuwa Uingereza ni mshirika moja kwa moja katika jinai zinazotekelezwa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina. Adnan Ghaith, mkuu wa mkoa wa Quds amesema katika kuwadia mwaka wa 104 wa kutangazwa Azimio la Balfour kwamba azimio hilo ni chanzo cha kutekelezwa jinai kubwa zaidi katika ulimwengu wa sasa na hivyo kuitaka Uingereza iwaombe msamaha Wapalestina kutokana na ukatili unaofanywa dhidi yao na Wazayuni wasio na utu.
Nukta inayobainika wazi katika Azimio la Balfour ni kwamba ni nembo ya ukoloni wa Magharibi Asia Magharibi kwa sababu lilitangazwa na dola la kikoloni. Kuhusu suala hilo, washiriki wa kongamano lililoandaliwa karibuni na Baraza la Kitaifa la Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO huko Aman mji mkuu wa Jordan kwa mnasaba wa kuwadia mwaka wa 104 wa kutangazwa Azimio la Balfour wamesisitiza kuwa jinai ya Balfour ulikuwa mwanzo wa siasa za wakoloni ambazo ziliweka msingi wa kutekelezwa jinai zingine zote dhidi ya Wapalestina, na ambazo zimelipelekea kufukuzwa zaidi ya nusu ya Wapalestina kutoka ardhi zao na mamia ya wengine kuuawa kinyama.
Suala jingine ni kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya wakoloni wa zamani na utawala wa hivi sasa wa Israel ambapo wakoloni hao ambao walichangia pakubwa katika kubuniwa utawala haramu wa Israel hivi sasa wangali wanauunga mkono kwa hali na mali utawala huo. Uingereza ilikuwa na nafasi muhimu katika kubuniwa utawala huo na leo Marekani imetokea kuwa mmoja wa waungaji mkono wakuu wa utawala huo na hasa katika kipindi cha rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump ambapo tuliona serikali yake ikitoa huduma kubwa na isiyo na mfano wake kwa Wazayuni kupitia mipango ya kiusaliti dhidi ya taifa la Palestina kama vile ‘Muamala wa Karne’ na kuhamishiwa mjini Quds ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv.
Ni kwa msingi huo ndipo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas ikasema kwa mnasaba wa kuwadia mwaka wa 104 wa kutangazwa Azimio la Balfour kwamba hakuna tofauti yoyote iliyopo kati ya azimio hilo na mipango mingine inayoratibiwa na maadui dhidi ya Wapalestina.
Nukta nyingine muhimu kuhusiana na kuwadia kwa mwaka wa 104 wa azimio hilo ni hali ya mambo inayotawala sasa katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambapo mvutano na mtafaruku uliojitokeza katika serikali ya Tel Aviv umeandaa mazingira ya kukandamizwa na kutendewa jinai zaidi taifa madhlumu la Palestina. Mwenendo wa kufedhehesha na kiusaliti wa nchi za Kiarabu wa kuwa na uhusiano wa kawaida na maghasibu Wazayuni ni suala jingine ambalo limepelekea kuongezeka jinai dhidi ya Wapalestina wasiokuwa na mtu wa kuwatetea. Kwa ibara nyingine ni kuwa ushirikiano mkubwa wa wakoloni na hasa Marekani na utawala wa kigaidi wa Israel, kufanywa wa kawaida uhusiano wa nchi za Kiarabu na utawala ghasibu wa Tel Aviv na vilevile udhaifu wa ndani ya utawala huo ni mambo ambayo yamepelekea kuongezeka jinai za Wazayubi dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.
Suala muhimu katika uwanja huu ni kuwa mbinu bora na ya kistratijia zaidi ya Wapalestina katika kukabiliana na changamoto hiyo ni mapambano dhidi ya Israel na waungaji mkono wake wa Magharibi. Kuhusu hilo chama cha Hamas kimetoa taarifa kwa mnasaba wa mwaka wa 104 wa Aziomio la Balfur kikitangaza kuwa mapambano katika sura zake zote yataendelea kuwa chaguo pekee la kisheria kwa ajili ya kukabiliana na maghasibu wa Kizayuni na hii ni kutokana na ukweli kwamba limethibitisha kivitendo taathira yake kubwa dhidi ya maghasibu hao. Kimesema hakitalegeza msimamo kuhusu uamuzi wake wa kuendelea kupigania haki za taifa la Palestina na kuwafukuza maghasibu wote wa ardhi za Wapalestina kutoka kwenye ardhi hizo.