Ripota na mwanasoka wa zamani wa Uingereza amepinga ubaguzi wa rangi katika jamii ya nchi hiyo wakati wa utawala wa Malkia Elizabeth II aliyeaga dunia juzi Alkhamisi akiwa na umri wa miaka 96.
Baada tu ya kutangazwa kifo cha Malkia Elizabeth II, Trevor Sinclair ambaye sasa ni kocha na mtaalamu wa soka, ameandika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akipinga ubaguzi wa rangi katika jamii ya nchi hiyo wakati wa utawala wa Malkia Elizabeth.
Sinclair ameandika kuwa: “Ubaguzi wa rangi umekithiri nchini Uingereza, hivyo watu weusi na Waasia hawapaswi kuomboleza kifo cha Malkia Elizabeth.”
Mwanasoka huyo wa zamani na mweusi wa Uingereza alilazimika kufuta ujumbe huo kufuatia mashambulizi ya wazungu wa mrengo wa kulia, watetezi wa ufalme na vyombo vya habari vya Uingereza.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya Uingereza pia wanaamini kwamba, idadi kubwa ya watu hasa weusi wana hasira na chuki dhidi ya mfumo wa kifalme wa nchi hiyo, lakini kutokana na hofu ya kushambuliwa na kupoteza nafasi zao za kazi, ni wachache tu miongoni mwao wanaohuthubutu kueleza hisia zao.
Ubaguzi wa rangi umekuwa tatizo kubwa kwa raia wa nchi za Ulaya. Kuenea ubaguzi wa rangi katika nchi tofauti za Ulaya zikiwemo Ufaransa na Uingereza hususan katika miaka michache iliyopita, kumewafanya raia wengi wa nchi hizo waandamane kupinga sera za ubaguzi barani humo.