Itamar Ben-Gvir, mzayuni mwenye misimamo ya kufurutu mpaka na kiongozi wa chama cha Nguvu ya Kiyahudi ambaye amependekezwa kuwa waziri wa usalama wa ndani katika baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu, ametangaza kuwa, mnamo siku chache zijazo ataushambulia Msikiti wa Al-Aqsa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Falastin Al-Yum, Ben-Gvir, amesisitiza katika mahojiano ya televisheni akisema: “mnamo siku chache zijazo na katika wakati ambao hautatangazwa hadharani, nitauvamia msikiti wa Al-Aqsa na jambo hili litafanywa kwa uratibu wa polisi wa Israel”.
Hayo yanajiri licha ya kwamba duru za usalama za utawala wa Kizayuni wa Israel tokea hapo awali zilikuwa zimetahadharisha kuhusu matokeo mabaya ya kuchaguliwa Ben-Gvir kuwa waziri wa usalama wa ndani katika baraza la mawaziri la Netanyahu.
Duru za Kizayuni zinaamini kuwa Itamar Ben-Gvir atachukua hatua zitakazovuruga hali ya mambo katika msikiti wa Al-Aqsa, mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na eneo zima kwa ujumla.
Katika jibu ililotoa kuhusiana na kauli ya mzayuni huyo mwenye misimamo ya kufurutu mpaka, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina, HAMAS imesisitiza kuwa: mpango wa Itamar Ben-Gvir wa kubadilisha hali ya Msikiti wa Al-Aqsa utashindwa na kugonga mwamba.
Sheikh Ikrima Sabri, Khatibu wa Msikiti wa Al-Aqsa naye pia amesisitiza katika hotuba yake kuwa: wananchi wa Palestina hawatamruhusu Ben-Gvir auvunjie heshima msikiti wa Al-Aqsa!.