Sanamu la afisa mkoloni wa zamani wa Ujerumani limeondolewa katika mji mkuu wa Namibia, Windhoek kutokana na mashinikizo ya wanaharakati wa nchi hiyo ya Kiafrika.
Sanamu la Curt von François, afisa mkoloni wa Ujerumani aliyekuwa na misimamo ya kutatanisha lilisimikwa huko Windhoek mwaka 1965, ili kumuenzi eti kama muasisi wa mji huo.
Hata hivyo kwa muda mrefu sasa, wanaharakati wa Namibia wamekuwa wakitaka kuvunjwa sanamu hilo, wakisisitiza kuwa linatonesha kidonda na kukumbusha juu ya ukandamizaji na dhulma zilizofanywa na Mkoloni Mjerumani katika enzi za ukoloni nchini humo.
Mwanaharakati Hildegard Titus amewaambia waandishi wa habari baada ya kuangushwa sanamu hilo kuwa, “Tumefurahi sana kwa kuondolewa sanamu la Von François. Amekuwa akitambulika kimakosa kama muasisi wa Windhoek, lakini ukweli ni kuwa sanamu lake ilikuwa nembo ya dhulma za kikoloni.”
Mei mwaka jana, Ujerumani kwa mara ya kwanza ilikiri hadharani kwamba ilifanya mauaji ya kimbari wakati wa ukoloni wake nchini Namibia, na kuahidi kutoa msaada wa zaidi ya euro bilioni moja na kusaidia miradi ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kama fidia ya jinai zake hizo.
Wakoloni wa Ujerumani waliua kwa umati makumi ya maelfu ya watu wa makabila ya Herero na Nama kwenye mauaji ya kuangamiza kizazi yaliyotokea baina ya mwaka 1904 na 1908; na hayo kuhesabiwa na wanahistoria kuwa mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20. Jinai hiyo ya Wajerumani ilivuruga uhusiano wa Namibia na Ujerumani kwa miaka mingi.
Zamani Namibia ilikuwa inajulikana kwa jina la Ujerumani ya Kusini Magharibi mwa Afrika wakati ilipokoloniwa na Wajerumani kuanzia mwaka 1884 hadi 1915.