Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la kujadili maendeleo ya tasnia ya habari nchini.
Kongamano hilo limeandaliwa na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, likishirikiana na wadau mbalimbali litakafanyika Jumatano Juni 29 kuanzia saa 2 asubuhi katika ukumbi wa SMJC, Mikocheni.
Amidi wa SJMC, Dk Mona Mwakalinga amewaambia wanahabari leo Jumapili Juni 26,2022 kuwa kongamano hilo, pia litajadili ushiriki wa SJMC katika tasnia ya habari nchini kwenye muktadha wa ushirikiano, changamoto, fursa za kuweza kufanya kazi pamoja kwa udhabiti zaidi kwa manufaa ya Taifa
Kwa mujibu wa Dk Mwakalinga, kongamano hilo ni sehemu ya maadhimisho ya kushehekea miaka 60 ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, huku akiwaalika wadau mbalimbali kuhudhuriwa wakiwemo waliosoma SJMC.
Dk Mwakalinga amewataja miongoni mwa wazungumzaji katika kongamano hilo kuwa ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Bakari Machumu, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.
Wengine ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Tido Mhando, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa- Zanzibar), Dk Mzuri Issa Ali, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Abdulmajid Nsekela na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk Ayoub Rioba.
Dk Mwakalinga amesema kaulimbiu ya kongamano hilo ni miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ‘ushiriki wa SJMC katika tasnia ya habari nchini.
Amesema kaulimbiu hiyo imechagizwa na mabadiliko yaliyofanyika ndani ya chuo kikuu cha Dar es Salkaam kwa miaka 60 tangu kuanzishwa kwake.
“Katika mabadiliko haya iliyokuwa shule ya uandishi wa habari nchini (TSJ) ilihuishwa na kuwa kitengo ndani ya chuo kikuu kama Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (IJMC) na kuanza kutoa elimu ya ngazi ya shahada za awali na uzamili, baadaye ikawa SJMC.
Dk Mwakalinga amefafanua kuwa zaidi ya washiriki 400 wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo kutoka ndani ya nchi na nje ya nchi wakiwemo viongozi wa Serikali, mawaziri, wabunge, maofisa uhusiano kwa umma, asasi za kiraia na maofisa habari wa Serikalini.
“Kongamano hili lina nafasi maridhawa katika kuanisha na kuanzisha ushirikiano mpya kati ya wadau wa kitaifa na kimataifa katika sekta ya habari,” amesema Dk Mwakalinga.