Kiongozi wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon anasema harakati hiyo ilikataa mapendekezo kadhaa ya hongo ya kifedha ya Marekani ili kusitisha mapambano yake na utawala wa Kizayuni wa Israel .
Katika mahojiano ya aina yake yaliyorekodiwa miaka 20 iliyopita na kurushwa hewani wiki hii, Katibu Mkuu wa Hezbollah Sayyed Nasrallah anasema harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu au muqawama ilikataa mapendekezo kadhaa ya Marekani ya fedha na kutambuliwa rasmi ili ijiondoe katika kadhia ya mgogoro wa Waarabu na Waisraeli.
Kanali ya Televisheni ya Al Mayadeen inarusha hewani vipindi vitano vilivyopewa anwani ya “40 na Zaidi” kuhusu harakati ya Hizbullah. Vipindi hivyo vinarushwa hewani kwa mnasaba wa kumbukumbu ya miaka 40 ya kuanzishwa Harakati ya Hezbollah na pia kumbukumbu ya miaka 30 ya kuchaguliwa Sayyid Hassan Nasrallah kama mkuu wa harakati hiyo. Vipindi hivyo ni pamoja na mahojiano yaliyorekodiwa kitambo lakini ambayo hayajawahi kurushwa hewani baina ya Sayyid Nasralllah na Ghassan Ben Jeddou, Mkurugenzi Mtendaji wa sasa wa al-Maydeen.
Katika sehemu ya tatu ya vipindi hivyo, Nasrallah anasema Marekani ilitoa ofa kadhaa kwa Hizbullah baada ya ukombozi wa kusini mwa Lebanon na eneo la magharibi mwa Bekaa mnamo 2000, ikilenga kuleta mabadiliko katika harakati hiyo na kuiondoa kabisa katika kadhia ya mgogoro wa Waarabu na Israel.
Marekani ilijaribu kuishawishi Hezbollah kwamba hakuna haja ya mapambano kuhusu mashamba ya Shebaa yaliyokuwa yakikaliwa kwa mabavu na Israel na kwamba kadhia hiyo ingeweza kutatuliwa kwa mazungumzo, amesema Sayyid Nasrallah.
Kwa mujibuwa wa Sayyid Nasraellah, kile ambacho Marekani ilikuwa ikitoa kwa Hizbullah mkabala wa harakati hiyo kusitisha mapambano ni pamoja na suluhisho kuhusu suala la wafungwa wa Lebanon katika magereza ya Israel, kutambua jukumu la kisiasa la Hizbullah na kuingizwa Hizbullah serikalini, kuipa harakati hiyo misaada ya kifedha ya kujenga tena maeneo yaliyokombolewa na kuiondoa Hizbullah kwenye orodha ya Marekani ya eti makundi ya kigaidi.
Sayyid Nasrallah pia amefichua kuwa Marekani ilikuwa inataka Hizbullah isitishe uungaji mkono wake wa kifedha na kijeshi kwa harakati za ukombozi wa Palestina.
Hezbollah ilianzishwa kufuatia uvamizi wa Israeli kusini mwa Lebanon mwaka 1982 na tangu wakati huo, harakati hiyo imestawi kwa kasi na kupata nguvu kubwa za kijeshi na kiisasa.