Nasrullah: Macho na makombora yetu yameelekezwa kwenye medani ya gesi ya Karish

Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah, amesema leo Jumamosi kwamba macho na makombora ya harakati hiyo yameelekezwa kwenye medani ya gesi ya Karish, ambao inazozaniwa baina ya Lebanon na utawala haramu wa Israel.

Sayyid Nasrullah amesema katika hotuba yake kwa njia ya televisheni kuwa “haiwezekani kuruhusu uchimbaji wa mafuta na gesi kutoka kwenye medani ya Karish kabla ya Lebanon kupata matakwa yake halali.”

Amesema: “Tunafuatilia mwenendo wa mazungumzo ya kuainisha mipaka ya bahari,” na kuongeza kuwa, “Kwetu, mstari mwekundu usiopaswa kuvukwa ni mwanzo wa uchimbaji wa mafuta na gesi kutoka medani ya Karish.”

Ameendelea kusema kuwa lengo la harakati ya Hizbullah ni kuhakikisha Lebanon inaweze kuchimba mafuta na gesi, na kwamba faili hilo halihusiani na faili jingine lolote.

Utawala ghasibu wa Israel unadai kuwa eneo lote la Karish liko katika eneo lake la kipekee la kiuchumi, wakati Lebanon inasisitiza kuwa medani hiyo iko katika sehemu ya maji inayozozaniwa.

Eneo hili lina futi za ujazo trilioni 203 za gesi, na utawala wa Kizayuni wa Israel unataka kulidhibiti na kuwa muuzaji wa gesi badala ya mtumiaji tu wa nishati hiyo na kulitumia kama nyenzo ya kisiasa na kiuchumi katika fremu ya sera zake za kupenda kujitanua.

Awali Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon alisema hatua za Israel katika eneo la machimbo ya gesi ya Karish ni ukiukaji wa mamlaka ya nchi hiyo na akaeleza bayana kuwa hakuna shaka yoyote muqawama unao uwezo wa kijeshi na kiusalama wa kumzuia adui mzayuni asichimbe mafuta na gesi katika eneo hilo.

Mapema mwezi Juni utawala wa Kizayuni wa Israel ulivuka mpaka wa baharini wa Lebanon na kuweka jukwaa la gesi katika Bahari ya Mediterania ukipanga kulitumia jukwaa hilo kuchimba mafuta na gesi eneo la machimbo ya gesi la Karish lililopo kwenye maji ya ardhi ya Lebanon.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *