Nchi kadhaa za Ulaya kutambua rasmi taifa la Palestina

Viongozi wa Ireland na Uhispania wametangaza kuwa nchi kadhaa za bara la Ulaya zinakaribia kutambua rasmi nchi huru ya Palestina.

Waziri Mkuu mpya wa Ireland Simon Harris na mwenzake wa Uhispania Pedro Sanchez siku ya Ijumaa walithibitisha kujitolea kwao “kutambua Palestina kama taifa haraka iwezekanavyo, wakati hali itakaporuhusu.”

Harris na Sanchez walitangaza hayo wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari katika Majengo ya Serikali huko Dublin.

Harris amesema mataifa ya Umoja wa Ulaya yalikubaliana mwezi uliopita kwamba yatachukua hatua ya kuitambua Palestina wakati masharti yakiwa sawa.

Ameongeza kuwa watu wa Palestina wanastahili heshima sawa na watu wengine duniani.

Iceland, Sweden, Poland, Jamhuri ya Czech na Romania ni miongoni mwa nchi ambazo tayari zimetoa utambuzi wa kisheria kwa taifa la Palestina.

Bunge la Norway lilipitisha azimio mwezi Novemba mwaka jana kuwa tayari kulitambua taifa huru la Palestina.

Tangu Oktoba 7, mamia kwa maelfu ya watu wameingia mitaani kote Ulaya katika kuonyesha mshikamano na Wapalestina wakati huu wa vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza uliozingirwa.

Tangu kuanza kwa mashambulizi hayo ya kinyama, utawala wa Israel umeua Wapalestina 33,634 na kuwajeruhi wengine karibu 76,214, wengi wakiwa ni wanawake na watoto. Utawala katili wa Israel unapata himaya madola ya Magharibi yakiwemo Marekani, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *