Netanyahu: Kama si msaada wa Saudia tusingeweza kupatana na Waarabu

Waziri Mkuu wa zamani wa utawala haramu wa Israel amesema kuwa, kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu kumefanikiwa kwa mwafaka na baraka za Saudi Arabia.

Benjamin Netanyahu amesema: “Jambo la kwanza ninalopaswa kukiri ni kwamba Saudi Arabia ilianza kutekeleza mpango wa kuanzishwa uhusiano baina ya Israel na nchi za Kiarabu hapo kabla, kwa sababu Riyadh ilifungua anga yake kwa mamia ya maelfu ya Waisraeli mwaka 2018 kabla ya kutiwa saini mapatano ya kuanzishwa rasmi uhusiano baina ya Tel Aviv na baadhi ya nchi za Kiarabu maarufu kwa jina la Abraham Accords hapo mwaka 2020. Netanyahu amesema uamuzi huo wa Saudi Arabia uliwawezesha maelfu ya Waisraeli kutumia anga ya Saudia na kuingia katika nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi.

Benjamin Netanyahu ameongeza kuwa: Makubaliano ya Abraham na Waarabu yasingewezekana bila ya ridhaa ya Saudi Arabia, kwa hiyo Riyadh inaelekea kuanzisha rasmi uhusiano na Israel.

Waziri wa Usafirishaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Merav Michaeli, hapo awali aliashiria mwelekeo wa Wasaudia wa kufanya mapatano na utawala huo, ambayo ni hatari kwa kadhia ya kupigania haki za taifa la Palestina na akasema: “Ushirikiano wa Tel Aviv na Riyadh -ambao ni sehemu ya mchakato wa mapatano baina ya Israel na nchi za Kiarabu – kuhusiana kupaa ndege za Israeli katika anga ya nchi hiyo, unaendelea.

Wakati huo huo serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani inafanya jitihada kubwa za kuhakikisha kwamba Saudi Arabia inaanzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni wa Israel; suala ambalo lilifichuliwa kwa mara ya kwanza na tovuti ya “Axios” mwezi uliopita. Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni pia hivi karibuni vilichapisha ripoti nyingi kuhusu mabadiliko yaliyojitokeza katika uhusiano wa Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel.

Harakati za kupigania uhuru za Palestina zimelaani vikali hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha au kutaka kuanzisha uhusiano rasmi na utawala ghasibu wa Israel unaokalia kwa mabavu Quds tukufu na kibla cha kwanza cha Waislamu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *