New York Times: Iran imekuwa msafirishaji nje mkubwa wa drone duniani

Gazeti la The New York Times la Marekani limewanukuu wataalamu mbalimbali wakisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa msafirishaji nje mkubwa wa ndege zisizo na rubani (drone) duniani na inazidi kueneza ushawishi wake katika maeneo tofauti ya hata nje ya Asia Magharibi.

Shirika la habari la FARS limelinukuu gazeti hilo la Marekani likidai kuwa, Iran inauza teknolojia ya drone kwa nchi zilizoko nje ya aneo la Asia Magharibi na inajitahidi kuwa na nafasi kubwa zaidi ya zana hizo, kimataifa.

Gazeti hilo la The New York Times aidha limesema, katika miaka ya hivi karibuni Iran imepiga hatua kubwa za mtawalia katika kubuni, kutengeneza na kuzalisha ndege zisizo na rubani za kijeshi na kuzipeleka katika nchi zilizoko nje ya ukanda wa Mashariki ya Kati.

Vile vile limedai kuwa, Iran inafanya juhudi za kuongeza ushawishi wake kimataifa na kwa hivi sasa inajaribu kuzipa nchi nyingine droni zake za kisasa za kijeshi zikiwemo nchi zilizowekewa vikwazo na Marekani kama vile Venezuela na Sudan.

Gazeti hilo la Marekani limedai pia kuwa, siasa hizo ni muhimu sana kwa Iran kwa ajili ya kudhamini uwezekaji na kuwa na ushawishi wa kisiasa wakati huu ambapo iko chini ya vikwazo vya Marekani.

New York Times limeongeza katika madai yake hayo kwamba, Russia ni mshitiri wa lazima wa silaha za Iran, likiashiria madai ya viongozi wa Marekani waliyoyatoa wiki za hivi karibuni waliodai kuwa, Russia ina nia ya kununua mamia ya ndege zisizo na rubani za Iran kwa ajili ya kuzitumia katika vita vyake nchini Ukraine.

Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kuwa, uhusiano wa kijeshi wa Tehran na Russia uko katika kiwango kile kile cha kabla ya kuanza vita vya Ukraine.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *