New York Times: Wapangaji wa mapinduzi walitaka kumuua Kansela wa Ujerumani

Gazeti la New York Times la Marekani limefichua kuwa wanachama wa kundi la mrengo wa kulia la “Reich Citizens” lililohusishwa na njama ya mapinduzi huko Ujerumani lilikuwa na nia ya kumuua Kansela wa nchi hiyo, Olaf Schultz.

Huku uvumi wa vyombo vya habari kuhusu mapinduzi yaliyofeli nchini Ujerumani ukiendelea kutapakaa, gazeti la New York Times limevinuu vyanzo ambavyo limedai ni vya kuaminika kwamba kumuua Olaf Schultz ilikuwa sehemu ya mpango huo wa mapinduzi.

Wiki moja baada ya kuchapishwa habari kuhusu kesi ya njama ya kundi la mrengo wa kulia la “Reich Citizens” ya kufanya mapinduzi nchini Ujerumani na kuiondoa madarakani serikali ya nchi hiyo, gazeti la Marekani la New York Times limeripoti kwamba maisha ya Kansela wa Ujerumani, Olaf Schultz yalikuwa hatarini kama njama hiyo isingezimwa.

Baada ya msako mkali wa kikosi cha usalama na polisi katika maeneo kadhaa nchini Ujerumani wiki iliyopita, ilifichuka kuwa kundi hilo lilinunua silaha za moto na lilipanga kushambulia Bunge la nchi hiyo.

Duru za usalama zinasema kuwa, maafisa 3,000 walifanya msako kwenye maeneo 130 ndani ya majimbo 11 kati ya 16 ya Ujerumani na kuwatia mbaroni makumi ya washukiwa wa njama hiyo ya mapinduzi.

Katika ripoti yake, gazeti la New York Times limenukuu vyanzo vitatu vya karibu na uchunguzi kuhusiana na jaribio la mapinduzi la kundi hilo, ambavyo vimesema kwamba wapangaji wa njama hiyo walipanga kumuua Kansela wa Ujerumani, Olaf Schultz.

Vyanzo vya New York Times pia vimedai kwamba “Heinrich XIII” anayedaiwa kuwa kiongozi wa kundi la mrengo wa kulia “Reich Citizens” angechukua udhibiti wa Ujerumani iwapo mapinduzi hayo yangefanikiwa.

Waziri wa Sheria Marco Buschmann ameiita misako hiyo kuwa ni operesheni ya kupambana na ugaidi, akiongeza kuwa washukiwa hao huenda walipanga kufanya shambulizi la silaha dhidi ya taasisi za serikali. Waendesha mashitaka wamesema washukiwa hao wanahusishwa na vuguvugu linalofahamika kama Reich Citizens ambalo wafuasi wake wanapinga katiba ya sasa ya Ujerumani na wanataka serikali iangushwe.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *