Nigeria ; Waislamu waandamana kulaani mauaji ya kimbari nchini Yemen na jinai za muungano vamizi uliopo chini ya uongozi wa Saudi Arabia

Katika kuitikia wito wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Waislamu nchini Nigeria wameandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo Abuja, kulaani jinai za muungano vamizi unaoongozwa na utawala wa Saudi Arabia ambao umeendelea kutenda jinai na mauaji ya kimbari nchini Yemen.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu yenye jumbe mbalimbali wametangaza himaya na uungaji mkono wao kwa wananchi wa Yemen na wakati huo huo kulaani jinai za Saudi Arabia na washirika wake huko Yemen.

Waislamu wa Nigeria sambamba na kujiita kuwa wao ni Wayemen wamesisitiza haja ya kukomeshwa jinai na mauaji ya kizazi dhidi ya taifa la Yemen.

Waandamanaji hao wameitaka jamii ya kimataifa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kujitokeza na kuchukua hatua za kuhitimisha mauaji ya kila leo ya utawala wa Aal Saud na washirika wake dhidi ya wananchi wa Yemen wasio na ulinzi.

Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa, jinai zinazofanywa na ukoo wa Aal Saud nchini Yemen zinafanana kikamilifu na jinai za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi madhuluumu wa Palestina.

Utawala wa kifamilia wa Saudi Arabia huku ukiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa ulianzisha hujuma na mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen Machi 2015 na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, anga, na nchi kavu.

Vita hivyo aidha hadi sasa vimeuwa makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen na kuwafanya mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi, mbali na kuharibu asilimia kubwa ya miudomsingi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu na kuifanya nchi hiyo kukabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *