Nigeria yaomba kuwa na ushirikiano wa kijeshi na Iran

Mwanadiplomasia mstaafu na mzoefu wa Nigeria Babaji Umar Misau amesema, ana matumaini kuwa nchi yake itaendelea kuwa na ushirikiano mzuri na wenye manufaa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo rafiki yake wa zamani kama ilivyokuwa kwa miongo mingi.

Misau ambaye ni balozi wa zamani wa Nigeria katika nchi za Burkina Faso, Kenya na Somalia, amezungumzia umuhimu wa hati ya makubaliano iliyotiwa saini kati ya Tehran na Abuja kwa lengo la Iran kusaidia kukarabati vinu vya kusafisha mafuta vya Nigeria na kubainisha kwamba, kusainiwa kwa hati hiyo kunaonyesha kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeendelea kuwa mzuri kwa miaka yote hii.
Akizungumza katika mahojiano na mwandishi wa habari wa Iranpress mwanadiplomasia huyo wa zamani wa Nigeria amesisitiza kuwa, bila kuwa na maelewano mazuri, haiwezekani kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na kupanua uhusiano wa kiuchumi na kisiasa.
Babaji Umar Misuwu aidha amesema kuhusu ombi la serikali ya Nigeria kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran la kutaka kuimarishwa uhusiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili, kwamba Iran itaweza kuisaidia Nigeria katika uga wa zana za kijeshi au utoaji mafunzo.
Tarehe 24 ya mwezi uliopita wa Agosti, Bashir Magashi, Waziri wa Ulinzi wa Nigeria, alikutana na Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Abuja Mohammad Ali Bak, ambapo wawili hao walizungumzia haja ya kupanuliwa ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi mbili.
Magashi alisema, mapendekezo kadhaa yametolewa kwa ajili ya kuboresha uhusiano wa kijeshi kati ya Nigeria na Iran.
Kwa upande wake, Mohammad Alibek alisema katika mazungumzo hayo kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaisaidia Nigeria ili kuhakikisha amani na usalama zinarejea nchini humo.
Hivi karibuni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Nigeria zilitia saini hapa mjini Tehran hati tisa za ushirikiano katika nyuga tofauti za utamaduni, utalii, mafuta, kilimo, michezo na biashara.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *