Norway yakata ushirikiano na mashirika yanayoiunga mkono Israel

Mfuko wa Taifa wa Utajiri wa Norway umetangaza kuwa unakata ushirikiano uliokuwepo baina yake na makampuni yanayouunga mkono utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Mfuko wa Taifa wa Utajiri wa Norway umeishauri wizara ya fedha ya nchi hiyo kusitisha uwekezaji katika baadhi ya makampuni, yanayousaidia utawala wa Israel katika kukiuka haki za Wapalestina na kuendeleza ukaliaji wa mabavu wa ardhi zao.
Mfuko wa Taifa wa Utajiri wa Norway unapanga kuweka vigezo vigumu zaidi vya maadili ili kusitisha ushirikiano na baadhi ya makampuni ambayo yanausaidia utawala ghasibu wa Israel katika vita vya Ghaza, na kuondoa hisa zake katika makampuni hayo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mfuko wa Utajiri wa Norway ambao kutokana na kuwa na akiba ya dola trilioni 1.7 ndio mfuko mkubwa zaidi wa uwekezaji duniani, unapanga pia kupitia upya hisa zake katika makampuni yanayofanya kazi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Kuhusiana na suala hilo, makampuni ya utengenezaji silaha ya Marekani nayo pia yatachunguzwa.
Inasemekana kuwa, mtoa uamuzi wa mwisho katika suala hilo ni Baraza la Benki Kuu ya Norway; lakini kwa mujibu wa barua ya Baraza la Maadili la Mfuko wa Utajiri wa Norway kwa Wizara ya Fedha ya nchi hiyo, si makampuni mengi yatakayoathiriwa na uamuzi huo.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *