OIC yaitisha kikao cha dharura kujadili hujuma za Israel dhidi ya msikiti wa al-Aqswa

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetangaza kuwa, wiki hii itaitisha kikao cha dharura cha nchi wanachama kwa ajili ya kujadili hujuma za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya msikiti wa al-Aqswa.

Duru za karibu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC)  zinasema kuwa, kikao hicho cha dharura kinatarajiwa kufanyika kesho Jumanne katika makao makuu ya jumuiya hiyo mjini Jeddah huko nchini Saudi Arabia.

Sehemu nyingine ya taarifa ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeeleza kuwa, kikao hicho cha dharura kimeitishwa kutokana na kushadidi hujuma mtawalia za utawala haramu wa Israel katika mji wa Quds na kuvunjiwa heshima mara kwa mara msikiti mtakatifu wa al-Aqswa.

Itamar Ben-Gvir, Waziri mpya wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni, Jumanne iliyopita, na ikiwa ni katika wiki yake ya kwanza ya kazi akiwa na kundi jingine la Wazayuni waliokuwa wanasindikizwa na jeshi la utawala huo ghasibu, walifanya uchochezi mkubwa na kuuvunjia heshima Msikiti wa al-Aqsa kwa kuingia msikitini humo bila kujali lolote.

Msikiti wa Al-Aqsa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho muhimu wa Kiislamu na Palestina mjini Beitul Muqaddas na utawala wa Israel unajaribu kuharibu umuhimu huo, lakini kusimama na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala wa Kizayuni na kuufanya ushindwe kufikia malengo yake maovu dhidi ya Waarabu na Waislamu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *