Ongezeko la maneno ya kibaguzi dhidi ya Waafrika katika Twitter

Ongezeko la matumizi ya maneno ya kibaguzi dhidi ya watu wenye asili ya Afrika kwenye mtandao wa Twitter kufuatia umiliki mpya wa kampuni hiyo ni jambo ambalo limeibua hoja ya kuzitaka kampuni za mitandao ya kijamii kuwajibika zaidi kuhusu chuki inayoelekezwa dhidi ya watu hao.

Hayo yamesemwa  na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu kupitia taarifa yao waliyoitoa Jumamosi huko Geneva, Uswisi. Wataalamu hao wamesema neno hilo la Kiingereza linaloanza na herufi ya “N” limezidi kutumika katika siku za karibuni kwenye mtandao huo.
“Katika siku za mwanzo za umiliki mpya wa kampuni hiyo hivi karibuni, Mtandao wa Utafiti katika Chuo Kikuu cha Rutgers nchini Marekani umesema matumizi ya neno hilo yameongezeka kwa asilimia 500 ndani ya saa 12 ikilinganishwa na kipindi cha mmiliki aliyetangulia,” wamesema wataalamu hao.
Wamesema ingawa Twitter ilidai kuwa takwimu hizo ziliongezeka kutokana na kampeni ya makusudi iliyoendeshwa na baadhi ya watu na kwamba hakuna fursa ya chuki, maelezo yoyote ya chuki dhidi ya watu wenye asili ya Afrika yanatia shaka kubwa na lazima hatua zichukuliwe kwa misingi ya haki za binadamu.
Wataalamu hao wamesema kauli za chuki, chuki kwa misingi ya masuala ya uzawa, rangi na dini kwenye mitandao ya kijamii sio tu jambo linalotia hofu kwenye Twittter pekee bali pia majukwaa mengine makubwa ya mitandao ya kijamii kama vile Meta (Facebook). Ingawa baadhi wanadai kutoruhusu kauli za chuki bado kuna pengo kati ya ahadi za kampuni na sera na usimamizi wake.”
Utafiti wa hivi karibuni kutoka taasisi ya Global Witness na SumOfUs umedhihirisha ni kwa vipi kampuni ya Meta inayoendesha Facebook inashindwa kuzuia matangazo ya chuki dhidi ya watu wenye asili ya Afrika.

Wamesema licha ya Meta kuchukua hatua ya kuunda Bodi ya ufuatiliaji wa maudhui mwaka 2020, bado matokeo yake kwa sasa hayajaonekana pengine siku za usoni.
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu Volker Türk hivi karibuni aliandika barua ya wazi kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Twitter Elon Musk akisisitiza kuwa uhuru wa kujieleza si kibali cha kusambaza taarifa za uongo zenye madhara ambazo zinaleta madhara halisi duniani.
“Alikumbusha kuwa sheria ya Haki za binadamu iko dhahiri – Uhuru wa kujieleza hukoma pale chuki inapochochea ubaguzi, uhasama au ghasia,” wamesema wataalamku hao wakiongeza kuwa mara kwa mara wanaona kusambaa kwa chuki na kauli za chuki dhidi ya watu wenye asili ya Afrika na makundi mengine sio tu vinadumaza haki zao bali pia vinajenga mipasuko mikubwa kwenye jamii.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *