Onyo jipya la rais wa utawala wa Kizayuni kuhusu uwezekano wa kusambaratika utawala huo kutokea ndani.

Kufuatia mgogoro wa ndani wa utawala haramu wa Israel na kuzuka hitilafu kali ambazo zimechochewa na mpango wa mageuzi ya mahakama, Rais Isaac Herzog wa utawala huo kwa mara nyingine tena ameonya dhidi ya uwezekano mkubwa wa kusambaratika utawala huo wa kibaguzi.

Isaac Herzog ameeleza kuwa, ana wasiwasi mkubwa juu ya kile kinachoendelea katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na kuongeza kuwa: Katika kipindi cha miaka 75  hadi 80 ya uwepo wa Israel, tunakabiliwa na mtihani mkubwa utakaoainisha hatima yetu. Hivi sasa ninaona mipasuko mikubwa inayozidi kuongezeka kina na michungu na kwa hakika ninaona tabu kuifikiria kwa undani. Ukweli ni kwamba dola la Kiyahudi lilianzishwa mara mbili katika historia ya Israel na likaanguka mara mbili kabla ya kufikia mwaka wake wa themanini.

Maonyo hayo hayajatolewa na Herzog pekee, bali awali viongozi wengine wa utawala huo walikuwa wameonya mara kadhaa juu ya uwezekano wa kusambaratika Israel kutokea ndani kutokana na kina na kiwango cha migawanyiko iliyopo.

Mnamo Mei 2021, yaani, wakati vita vya siku 12 kati ya jeshi la utawala wa Kizayuni na makundi ya mapambano ya Palestina vilipoanza, Aryeh Shavit alichapisha kitabu kinachoitwa “Nyumba ya Tatu; Kutoka kwa Watu hadi Makabila” ambapo alichambua kushindwa Israeli katika nyakati tofauti katika kipindi cha miaka 70 iliyopita. Katika kitabu hicho amechunguza vitisho muhimu zaidi vinavyoukabili utawala huo wa Kizayuni, migogoro na mizozo ya ndani na jinsi ya kuwaunganisha Wazayuni kama fursa ya mwisho kwa Mayahudi.

Katika chapisho la kurasa 27 kwa Jumuiya ya Kizayuni mwezi Juni 2022, Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni alisema: Israel hivi sasa inakabiliwa na mtihani mkubwa na imesimama katika hatua ya kihistoria ambayo lazima iendelee, la sivyo, irejee katika kipindi cha machafuko. Hii ni kwa sababu leo, Israeli inashuhudia hali ambayo haijawahi kutokea tena huko nyuma na inakaribia kuporomoka. Sasa tunakabiliwa na hali hatari na ya kuainisha hatima. Huko nyuma, Israeli tayari ilikwishagawanyika mara mbili, kipindi cha kwanza cha mgawanyiko wake kilitokana na migogoro ya ndani katika miaka ya sabini na mara ya pili katika miaka ya 80 ya uwepo wake, na sasa tunaishi katika awamu ya tatu.

Kupitia makala, Ehud Barak, Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni pia ameweka wazi hofu yake ya kuangamia Israel kabla ya mwaka wa 80 wa kuasisiwa kwake na kusema: Mayahudi hawajawahi kutawala kwa zaidi ya miaka 80. Serikali ya sasa ya Israel inakaribia kuingia katika muongo wa nane wa uhai wake, na kuna hofu kwamba laana ya muongo wa nane itaipata serikali ya sasa ya Israel. Katika makala hiyo, ametaja baadhi ya serikali nyingine duniani zilizoathiriwa na laana ya muongo wa 80. Miongoni mwa serikali hizo ni Marekani iliyoingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe katika miaka ya 80 umri wake, Italia, ambayo ilikuwa nchi ya kifashisti katika kipindi hicho hicho, na Ujerumani ambayo iligeuka kuwa nchi ya kinazi na hatimaye kushindwa na kugawanyika sehemu mbili.

Tamir Pardo, mkuu wa zamani wa shirika la kijasusi la utawala ghasibu wa Israel, Mossad, ni afisa mwingine wa Kizayuni ambaye katika hotuba yake katika Chuo Kikuu cha Tel Aviv, ameidhihirisha Israel kuwa ni jamii inayojiangamiza yenyewe na kusema: Ingawa kuna mijadala mingi inayohadiliwa kuhusu vitisho vikubwa vinavyoikabili Israel, lakini tishio kubwa zaidi kwa Israeli ni Waisraeli wenyewe, na mchakato wa kujiangamiza jamii ya Israeli umekamilika katika miaka ya hivi karibuni. Israeli ni jamii inayojiangamiza yenyewe. Ukweli  wa mambo ni kwamba jamii ya Waisraeli imegawanyika na migawanyiko hiyo inaendelea kushuhudiwa wazi ambapo Waisraeli wanajishinda na kujiangamiza wenyewe.

Hata kama Netanyahu sasa anawapinga waandamanaji na wakosoaji wanaozungumzia kuporomoka Israel kutoka ndani, lakini yeye mwenyewe alitoa kauli sawa na hiyo mwaka 2017 ambapo alisema kwamba anajaribu kuifikisha Israel katika kumbukumbu ya miaka 100, lakini suala hilo haliko wazi kwa sababu hakuna dola la Kiyahudi lililowahi kuishi kwa zaidi ya miaka 80.

Hali hiyo inaonyesha wazi kwamba hata kama mivutano imeibuka kuhusiana na kile kinachotajwa kuwa mageuzi au mapinduzi ya mahakama na hivyo kupelekea utawala huo haramu kukabiliwa na migogoro ya ndani isiyo na mfano wake, lakini ukweli wa mambo ni kwamba hitilafu za ndani hazihusiani tu na suala hilo bali changamoto na nyufa za ndani ni kubwa mno.

Serikali ya Netanyahu inadai kuwa marekebisho ya mahakama yatakayofanywa yatapunguza kiwango cha Mahakama ya Juu kuingilia masuala ya kisiasa; lakini wakosoaji wanasema kuwa Netanyahu, ambaye mwenyewe anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi, anajaribu kukwepa mashtaka hayo kwa kufanya mabadiliko katika vyombo vya mahakama na hivyo kueneza ufisadi ndani ya utawala huo.

Upinzani unaamini kuwa lengo kuu la mageuzi yaliyopendekezwa na muungano unaotawala ni “kumwondolea Netanyahu mashtaka ya ufisadi katika kesi tatu ambazo ziko wazi dhidi yake” na, zaidi ya hayo, kumfungulia mlango mshirika wake Arieh Derei kugombea licha ya kupatikana na hatia ya ulaghai, kukwepa kulipa kodi na wizi, ili apate fursa ya kuhudumu tena katika nafasi ya waziri.

Katika hali kama hiyo, hakuna nafasi ya kati ambapo inaweza kudhaniwa kuwa wapinzani na wafuasi wa Netanyahu wanaweza kufikia maelewano, jambo ambalo linaashiria kushadidi migogoro ya ndani na kuimarika kwa dhana ya kusambaratika utawala wa kigaidi wa Israel kutokea ndani. Ukweli huo umeashiriwa na kusisitizwa mara kadhaa na Isaac Herzog, ambaye ameonya kuhusu hatari ya hali inayotawala hivi sasa ndani ya utawala huo ghasibu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *