Wabunge wa Misri, wameonya kuhusu njaa na ughali wa bidhaa nchini humo na kusisitiza kuwa Wamisri wamechoshwa na hali hiyo. Wameituhumu serikali kuwa imeshindwa kabisa kukabiliana na mfumuko wa bei uliokithiri nchini kuhusu bidhaa za msingi.
Sambamba na kuanza mwaka huu mpya wa 2023, bei ya jbidhaa za msingi imeongezeka maradufu katika masoyo ya Misri kwa kadiri kwamba raia wengi wa nchi hiyo wameshindwa kumudu gharama kubwa ya bidhaa hizo sokoni. Bei kubwa ya bidhaa za msingi kama vile mafuta, sukari, mchele na unga imewakasirisha sana raia na wabunge wa Misri na kuwafanya waikosoe serikali ambayo wanasema imeshindwa kudhibiti hali hiyo kutokana na usimamizi wake mbaya kwenye soko la bidhaa muhimu.
Kufuatia ongezeko hilo kubwa na la ghafla la bei ya bidhaa, wabunge wametaka Ali Al-Masilehi, Waziri wa Manunuzi na Biashara afutwe kazi, kutokana na kupungua kwa usambazaji wa bidhaa za msingi sokoni na kuongezeka bei ya bidhaa hizo kila siku pamoja na utendaji mbaya wa mashirika ya udhibiti na usimamizi ya serikali.
Takwa hilo lilitolewa na wabunge hao katika kikao cha Jumanne iliyopita, kilichofanyika kwa ajili ya kuchunguza sababu za kupanda ghafla kwa bei na kuadimika kwa baadhi ya bidhaa muhimu katika masoko ya nchi hiyo.
Ahmed Farghal, mmoja wa wabunge hao, amesema wanaitaka serikali nzima ya nchi hiyo ijiuzulu kwa sababu sasa imekuwa ni wizara ya soko jeusi la magendo na hivyo kuwafanya wananchi wa Misri kupitia machungu makubwa kutokana na ughali wa bidhaa za msingi.
Kulingana na takwimu rasmi, theluthi moja ya watu wa Misri wanaishi katika hali ya umaskini. Uchumi wa nchi hiyo bado ni mbaya licha ya kupita zaidi ya muongo mmoja tangu mapinduzi ya Misri yafanyike Januari 25, 2011.